NA MARYAM HASSAN

UPANDE wa mashitaka wa serikali umepinga kupewa dhamana mshitakiwa Shija Makenzi Lufilisha (45) mkaazi wa Kidimni kwa sababu kiwango alichoshitakiwa nacho ni kikubwa.

Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Ayoub Nassir Sharif, alisema mshitakiwa amekamatwa na majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi yenye uzito wa gramu 4.2 kiwango ambacho ni kikubwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya mshitakiwa huyo kuomba kupewa dhamana kwa kosa aliloshitakiwa nalo.

Pingamizi hizo, amezitoa mbele ya Hakimu Khamis Ali Simai, wakati shauri hilo lilipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza.

Ombi hilo, lilipingwa vikali na wakili huyo na badala yake aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi kwa sababu upelelezi umekamilika.

Alidai kuwa tukio hilo alitenda Oktoba 6, mwaka huu, majira ya saa 8:00 za usiku huko Kidimni wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.