WASHINGTON,MAREKANI

POLISI  wa zamani wa Marekani aliyeshitakiwa kwa mauaji ya mwanamme mweusi ambaye hakuwa amejihami George Floyd ameachiliwa kutoka jela kwa dhamana.

Derek Chauvin alitoa Bondi ya dola milioni moja sawa na (Euro 774,000) na kuachiliwa,nyaraka za mahakama zinaonesha.

Ofisa huyo mzungu alirikodiwa kwenye kanda ya video akipiga goti kwenye Shingo ya Floyd kwa karibu dakika nane kabla ya kufariki dunia Mei 25.

Kifo cha Floyd kilisababisha maandamano makubwa nchini Marekani kushinikiza mageuzi katika idara ya polisi,yakiongozwa vugu vugu la Black Lives Matter.

Chauvin alifutwa kazi na sasa anasubiri hukumu dhidi yake baada ya kushitakiwa kwa mauaji ya kiwango cha pili na kuua bila kukusudia mwezi machi.

Maofisa wengine watatu J Alexander Kueng, Thomas Lane na Tou Thao pia walifutwa kazi na kushitakiwa kwa kutowajibika tukio la mauaji likifanyika mbele yao.

Maofisa wote wanne wanaotuhumiwa kwa mauaji ya Floyd huko Minneapolis, Minnesota, walilipa dhamana na wako huru wakisubiri hukumu dhidi yao kutolewa mwaka ujao.

Chauvin alikuwa anazuiliwa katika jela ya Oak Park Heights, Minnesota, tangu mwishoni mwa mwezi Mei.

Mnamo mwezi Juni, jaji aliweka dhamana ya dola milioni 1.25 bila masharti, ama dola milioni moja ambayo ilijumuisha masharti ya Chauvin kutowasiliana na familia ya Floyd, kupeana silaha yake na kutofanya kazi katika idara ya sheria ama ya usalama akisubiri hukumu dhidi yeke.