NA HAJI NASSOR, PEMBA

WANANCHI kisiwani Pemba, wameshauriwa kuvitumia vituo vya afya vilivyo karibu yao, kwa ajili ya kuwapeleka ndugu na jamaa zao, kufanyiwa uchunguuzi wa afya ya akili, badala ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji, kama ilivyo sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Chake Chake, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya afya ya akili duniani, Mratibu wa Huduma za Afya ya Akili Pemba Salim Khamis Ali, alisema wapo baadhi ya wananchi, huwapeleka ndugu na jamaa zao kwa waganga wa kienyeji.

Alisema wapo wagonjwa huwapokea wakiwa wameshacheleweshwa mno, kutokana na ndugu na jamaa zao, wanapowagundua kuwa wanaumwa hukimbilia kwa waganga wa kienyeji, jambo ambalo linawacheleweshea matatibu.

Mratibu huyo alisema, Wizara ya Afya Zanzibar katika kulijali kundi la watu wenye ugonjwa wa akili, imeweka huduma zao kwenye vituo vyote vya afya hadi vya vijijini.

Alisema hilo limewekwa, ili sasa kuwapunguzia masafa wagonjwa wa akili, wanaotaka huduma za afya ya akili, ambapo hapo zamani, walilazimika kwenda hospitali za Wilaya pekee.

“Ilikuwa huduma hizi za afya ya akili, zinapatikana hospitali za Wilaya za Wete, Mkoani na Chake Chake, lakini sasa hata kwenye hospitali za koteji na vituo vyote vya afya, huduma hizi zinapatikana,’’alieleza.

Mratibu huyo, alisema wagonjwa hao wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku kisiwani Pemba kutokana na msongo wa mawazo, au mtu kukumbwa na maradhi mengine kama vile Ukimwi.

“Hata magonjwa kama vile Ukimwi au mtu kuondokewa na mpendwa wake ghafla, haya yote yanaweza kusababisha kukumbwa na ugonjwa wa akili,’’alifafanua.