NA MARYAM HASSAN

KIJANA aliyeshitakiwa kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya ameachiliwa huru kwa sababu zaidi ya mwaka mmoja hakuna shahidi aliyefika mahakamani.

Kijana huyo ni Abdalla Khamis Juma (25) mkaazi wa Jendele ameachiliwa huru na Mahakama ya mkoa Mwera chini ya Hakimu Said Hemed Khalfan.

Abdalla alifikishwa mahakamani hapi kwa kosa hilo akiwa amepatikana na nyongo 23 alizokuwa amezihifadhi katika Mfuko wa plastik.

Hakimu huyo, alisema zaidi ya mwaka mmoja kesi hiyo ipo mahakamani na hakuna shahidi aliyefika, kwa hivyo hana budi kumuachia huru mshitakiwa huyo, ili aendelee na harakati zake za kimaisha.

Alisema sababu kubwa upande wa Mashitaka umeshindwa kuleta mashahidi licha ya kuwapa muda wa kuwasilisha mashahidi, jambo ambalo limesbabisha ameanza maisha ya uraiani baada ya kuachiliwa huru na Mahakama ya mkoa Mwera.

Kosa la kupatikana na dawa za kulevya anadaiwa kutenda Agosti 5, mwaka 2017, majira ya saa 12:15 za jioni huko Jendele wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja, ambapo ilidaiwa kuwa nyongo hizo kete 23, ambazo zinasadikiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya Heroin zina uzito wa gramu 0.4577 kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Kabla ya kutolewa kwa maamuzi hayo wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Ayoub Nassor, aliiambia mahakama kuwa hawajapokea shahidi.

Baada ya kutoa taarifa hiyo, aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupanga tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi, ombi ambalo lilipingwa na Hakimu wa mahakama hiyo.