NA MARYAM SALIM, PEMBA

UPANDE wa Mashtaka, umeiomba Mahakama ya Mkoa Chake Chake chini ya hakimu  Luciano Makoye Nyengo, kuliondosha shauri la mtuhumiwa Karama  Abdalla Machano miaka 35 mkaazi wa Chokocho, anayekabiliwa na tuhuma za kupatikana na misokoto 150 ya bangi, kutokana na hitilafu juu ushahidi.

Hakimu huyo alisema kuwa, upande wa Serikali umeomba mahakama iliondoshe shauri hilo, kutokana na kuwepo kwa tofauti wa ushahidi wa vielelezo na ushahidi uliotolewa na askari mpelelezi mahakamani hapo.

 “Sababu iliyowafanya na PP, juu ya kuondoshwa kwa shauri ni kutokana na utofauti uliojitokeza kutoka kwa mpelelezi, katika utoaji wa ushahidi wake mahakamani hapo,”alisema hakimu huyo.

 Hakimu huyu alisema kuwa, kumekuwa na utofauti wa ushahidi wa vielelezo vilivyofikishwa mahakani, kwani hapo mwanzo mpelelezi alidai ni misokoto 150, na badala yake alionesha misokoto 121 tu.

Shahidi huyo Polisi mpelelezi, mwenye namba ya usajili H 9159 D.C Fadhil, alieleza mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa alikamatwa na misokoto 150 ya bangi, ambapo katika kukitambua kielelezo akiwa anafunguwa na kuhesabu, hesabu zilikuwa tofauti na alizotaja kwenye hapo awali.