NA MWAJUMA JUMA

MRATIBU wa Mradi wa Malezi Mbadala mkoa wa Kaskazini Unguja, Nyezuma Simai Issa, amesema vitendo vya udhalilishaji wa watoto vitapungua endapo wananchi wataacha muhali na kuviripoti katika vyombo vya sheria.

Akizungumza na Wananchi wa shehia ya Mto wa Pwani wakati wa utoaji elimu ya ukatili na udhalilishaji kwa watoto, alisema muhali ndio chanzo cha watoto kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na kesi zake kushindwa kuendelea mbele kwenye vyombo vya sheria.

Alisema kupitia Mradi wa Malezi Mbadala unaotekelezwa na kijiji cha kulelea watoto yatima (SOS) kwa kushirikiana na Wizara ya Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto watahakikisha matendo hayo yanapatiwa ufumbuzi ili wananchi wawe na mwamko wa kuripoti kesi hizo.

Kwa upande wao Wananchi wa shehia hiyo walisema kesi kubwa katika kijiji chao zinazoripotiwa zaidi ni vitendo vya ubakaji kwa vijana, watoto na wazee hali inayowatia hofu kupata maambukizo.

Wamesema waathirika wakubwa ni watoto ambapo huharibiwa njia zao za uzazi kwani wapo chini ya umri wa miaka 18 na wengine huathirika kisaikolojia.

Hata hivyo wananchi hao walisema pia upo udhalilishaji wa utekelezaji wa familia ambao husababisha watoto kukosa haki zao za msingi na kupelekea kina mama kushindwa kumudu gharama za malezi peke yake na kupelekea watoto kudhalilishwa.

Jumla ya kesi 52 zimeripotiwa kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka huu katika wilaya ya Kaskazini ‘A’, Unguja ambazo ulawiti kesi mbili, shambulio la hatari mbili, shambulio la aibu tatu, kukashifu moja, ubakaji 34 na utelekezaji wa familia 10.

Shehia zilizoripotiwa kesi za udhalilishaji katika kipindi hicho ni Mto wa Pwani, Mkokotoni, Mkwajuni, Kidombo, Potoa, Kidoti, Chaani Kubwa, Uvivini Tumbatu, Jongowe, Donge Kipange, Donge Mchangani, Kivunge na Kikobweni mkoa wa Kaskazini.