NA AHMED MAHMOUD, ARUSHA
WANAWAKE nchini wametakiwa kujiamini wakitambua kuwa wao ni viongozi tokea ngazi ya familia hadi kwenye maeneo ya kazi zao za ujenzi wa taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi mstaafu na Mhadhiri wa chuo kikuu cha George Washngton Marekani, Liberata Mulamula, wakati akifungua kongamano la siku tatu la Chama cha wahasibu wanawake waliosajiliwa TAWCA jijini Arusha.

Alisema kuwa wanawake ni sehemu ya viongozi wanaojitambua tokea ngazi ya Familia na sio kwenye siasa pekee au kuangalia waliofanikiwa bali lengo kubwa ni kujitambua kuwa wanaweza.

“Tumekuwa tukidhani sana kuwa uongozi ni kwenye siasa tubadilike kwenye maeneo yote tulipo tufanye kazi zetu tukiamini kwenye uelewa wetu ndio msingi wa mafanikio yetu siku zote wala tusijione hatuwezi huyo ndio adui”

Naye  Mwenyekiti wa Chama hicho CPA Neema Kiure alisema chama hicho kimefanikiwa katika kipindi cha miaka mitano tokea kuanzishwa kwake mwaka 2015 kwa kufikia idadi ya takribani wanachama zaidi ya 500 nchi nzima.

Alisema lengo la kongamano hilo ni kuendelea kusaidia jamii ya wanawake nchini kuweza kujitambua na kuongeza uelewa wa majukumu yao ikiwa pia ni kusaidia vizazi vijavyo vya watoto wa kike kufikia malengo yao wakiwa mashuleni kupenda masomo yasiyopewa kipaumbele na wanafunzi katika shule mbalimbali nchini

Naye Mwenyekiti Mstaafu wa Chama hicho, Bahati Geuzye, alisema kuwa, mwamko unaoonekana leo ni sehemu ya juhudi za kila mmoja kuwa sehemu ya utendaji uliosaidia kufikia malengo toka wanachama 10 hadi zaidi ya 500.

Alisema kongamano hilo ni sehemu muafaka kuwaleta pamoja kujua changamoto na mafanikio yatakayowasaidia wanawake wahasibu waliosajiliwa kuendeleza na kujitambua ikiwa ni pamoja na kuihamasisha jamii ya watoto wa kike kupenda masomo ya hesabu.

Kwa Upande wake Afisa fedha Mkuu kutoka Shirika la ugavi wa Umeme nchini TANESCO, Renalta Ndege alisema kuwa msingi wa mafanikio ni uelewa na kutambua majukumu yao nao kama wanawake wanatambua hilo tokea ngazi ya familia.