KAMPALA, UGANDA

RAIS wa Uganda, anayejulikana kwa jina la Yoweri Kaguta Museveni, amebadilisha rasmi majina yake, kujumuisha jina lake la utoto linaliojulikana kama Tibuhaburwa.

Museveni alifanya uamuzi huo kufuatia sheria mpya iliyotolewa nchini humo ya kuwaruhusu raia kubadilisha majina.

Jina la Tibuhaburwa katika kabila lake la Banyankore, linaweza kutafsiriwa kama mtu ambaye hachukui wlaa kusikiliza ushauri, kuongozwa, kurekebishwa na wengine.

Hatua ya Museveni kubadilisha jina imezua uvumi na utani miongoni mwa Waganda katika mitandao ya kijaii, baadhi yao wakihoji kazi ya washauri wake.

Rais alisaini tamko kama inavyotakiwa na sheria ya usajili wa watu, ili kujulikana rasmi kama Yoweri Tibuhaburwa Kaguta Museveni.

Ingawa jina hilo limetajwa katika katika mazingira tofauti juu ya utawala wake wa miaka 34, hajawahi kulitumia hadharani.

Kulingana na hati ya upeanaji wa hati ya tarehe 6 Oktoba, rais anasema kwamba jina hilo limetumiwa kwenye vyeti vyake vya masomo.

Lakini inaaminika kuwa hatua hiyo inafuata mahitaji kutoka kwa Tume ya Uchaguzi, kwa wagombea wa uchaguzi 2021 kuhakikisha kuwa majina kwenye hati zao za uteuzi yanaingana na yale yaliomo kwenye rekodi zao za masomo.

Mnamo mwaka wa 2017, uamuzi wa mahakama ulibatilisha ushindi wa mbunge kwa misingi kwamba amebadilisha majina yake kwenye hati tofauti rasmi.