PHNOM PENH, CAMBODIA

WATU 13 wamefariki na wengine 12,376 wamehamishwa nchini Cambodia baada ya mvua za kitropiki zilizosababisha mafuriko kuleta madhara makubwa katika miji 19 na majimbo 25 ya ufalme huo.

Msemaji wa Serikali, Seak Vichet, alisema kuwa taarifa ya Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa (NCDM), ilisema kuwa tangu mwanzo wa mwezi, watu 193,268 wameathiriwa na mafuriko, na wengine 12,376 wamehamishiwa kwenye ardhi salama.

“Mafuriko yamesababisha vifo vya watu 13 hadi kufikia sasa, wakiwemo watoto watano,” aliiambia Xinhua, akiongeza kuwa majimbo yaliyoathiriwa zaidi ni pamoja na Battambang kaskazini magharibi, Pursat, na Banteay Meanchey pamoja na kusini mwa Kandal.

Taarifa zilisema kuwa Mafuriko hayo pia yameharibu vibaya nyumba 47,923 na hekta 186,689 za mpunga na mazao mengine kati ya hizo hekta za mahindi ni 12,958.

“Usafiri pia umevurugwa, kwani barabara kadhaa kuu katika majimbo yaliyoathiriwa zaidi zimefungwa ili kuzuia kuharibu zaidi maeneo mengine”, alisema msemaji huyo wa serikali.

Nae Waziri wa Hali ya Hewa, Lim Keanhor, alisema siku ya Alhamisi ilinyesha mvua kubwa, upepo, na mawimbi makubwa na kwamba mvua hizo zinatarajiwa kukatika Oktoba 19.

“Watu wanaoishi katika nchi tambarare, kando ya njia za maji na karibu na milima, wavuvi na wasafiri wa baharini wanapaswa kuwa waangalifu zaidi ili kuepuka hatari zozote zinazowezekana,” alisema katika taarifa kwa waandishi wa habari.

Nchi ya Cambodia kwa kawaida hupatwa na mafuriko ya mara kwa mara kufuatia mvuz za msimu zinazonyesha kati ya Agosti na Oktoba.

Mwaka jana, Mto Mekong ulifurika na kusababisha watu 30 kufariki kutokana na dhoruba.