RAMALLAH,PALESTINA

MWALIMU wa kike wa skuli ya wanawake ya Halima al Saadiyah ya Kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza huko Paletina Asma  Mustafa, ameshinda tunzo ya mwalimu bora duniani mwaka huu wa 2020 ijulikanayo kwa jina la Tuzo ya Elimu ya AKS.

Asma Mustafa ni Mwalimu wa lugha ya Kiingereza wa skuli hiyo ya wasichana na alipata tunzo hiyo ya mwalimu bora duniani baada ya kuwashinda washiriki wengi wa mashindano ya tunzo hiyo.

Alipata ushindi huo wa kupigiwa mfano kutokana na ubunifu wake katika usomeshaji na utunzi wa vitabu ikiwemo michezo 45 ya ufundishaji wa lugha ya Kiingereza kwa watu ambao Kiingereza si lugha yao ya asili.

Mwalimu huyo Mpalestina ni mwanachama wa taasisi nyingi za kimataifa za elimu na anafanya kazi pia na mashirika mbalimbali ya kimataifa kama vile Microsoft, Google, Apple na National Geographic. 

Jumuiya ya AKS Elimu ya nchini India mwaka jana pia ilitangaza majina ya walimu 100 bora duniani kutoka nchi 72 tofauti.

Miongoni mwa walimu hao bora ni Ayad Ahmad al Sufi mwalimu Mpalestina wa mjini Jenin, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kutokana na kazi kubwa ya kuyaingiza masomo katika mfumo wa kidijitali.

Rana Ziyada, mwalimu mwengine Mpalestina mkaazi wa Ukanda wa Ghaza naye alikuwa miongoni mwa walimu 50 bora duniani mwaka 2018. Licha ya kuzingirwa kila upande na kufanyiwa ukandamizaji mkubwa mno na utawala dhalimu wa Israel, lakini Wapalestina daima wamekuwa wakitia fora katika masuala ya elimu