NA KHAMISUU ABDALLAH

MWANAFUNZI aliyekimbia mahakamani kwa kipindi kirefu tokea Julai 25 mwaka 2019 kesi yake ilipohukumiwa amekamatwa tena na mdhamini wake na kurejeshwa mahakamani.

Oktoba 5 mwaka huu mshitakiwa huyo alifikishwa tena mahakamani hapo yeye na mdhamini wake, lakini kutokana na kutoonekana kwa jalada la kesi yake mahakamani hapo Hakimu mdhamini wa mahakama hiyo Mohammed Subeit, iliiahirisha hadi Oktoba 12 kwa ajili ya kutajwa.

Mshitakiwa huyo alihukumiwa mahakamani hapo na Hakimu Fatma Omar kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi tisa baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo dhidi ya shitaka linalomkabili.

Mahakama pia iliamuru pesa zilizowekwa kwa ajili ya dhamana zilitaifishwa mahakamani hapo.

Mwanafunzi huyo alitambulika kwa jina la Mundhir Rajab Juma (20) mkaazi wa Kidongochekundu wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo awali alikuwa akikabiliwa na shitaka la shambulio la kuumiza mwili kinyume na kifungu cha 247 cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.