HARARE, ZIMBABWE

MWANDISHI wa habari kutoka Zimbabwe, Hopewill Chin’ono ameelezea namna alivyokabiliana uso kwa uso na athari za kusaidia kufichua kashfa ya rushwa mwanzoni mwa mwaka huu.

Alisema, Julai 20 mwaka huu majira ya asubuhi, wanaume nane baadhi yao wakiwa na silaha aina ya AK-47, waliwasili kwenye geti la nyumba yake, wakiwa na gari ambalo halikutambulika mara moja.

Alisema alipelekwa gerezani kwa muda wa mwezi mmoja, ambako wafungwa hawakuwa na barakoa kabisa, hakukuwa na maji ya kutiririka wala sabuni kwenye vyumba vya gereza, ambapo walifungiwa humo saa 17 kwa siku.

Alieleza sababu ya hayo ni baada ya kuchapisha taarifa za kashfa ya ugavi kuhusu mamilioni ya dola za kupambana na Covid-19, iliyohusisha mikataba ya manunuzi ya vifaa kwa gharama kubwa, ambapo waziri wa afya baadae alifukuzwa kazi na sasa anakabiliwa na kesi kuhusu shutuma hizo.

Wakati alipokamatwa msemaji wa serikali alisema hakuna kazi iliyo juu ya sheria, hivyo anafikiri kuwa nia ya kukamatwa kwake ni kuwatisha waandishi wa habari, ambapo mpango wao huo unaonekana kufanikiwa.

Mwandishi huyo alisema miaka mitatu tangu Robert Mugabe kuondolewa madarakani, vitendo vya kutekwa kwa watu waliokuwa wakosoaji wa serikali vimekuwa kawaida.

“Sio kwamba hakukuwa na vitisho chini ya utawala wa Mugabe, lakini nilikuwa nina uwezo wa kuripoti taarifa bila kukamatwa, ikiwemo makala yangu iliyopata tuzo iliyozungumzia vurugu za baada ya uchaguzi mwaka 2008” alisema Chin’ono.