NA MARYAM HASSAN

 MWENYEKITI wa CCM wilaya ya Dimani Hussein Ali Kimti amesema ushindi wa CCM umekuja kufuatia viongozi wake kutekeleza vyema ilani ya chama hicho.

Hayo aliyasema mara baada ya kutolewa matokeo ya uwakilishi na udiwani kwa wilaya ya Magharibi ‘B’ ambapo CCM iliibuka kidedea kwa nafasi zote.

Hayo aliyasema skuli ya Kiembesamaki Sekondari wakati akizunguza na Zanzibar Leo, mara baada ya Tume ya Uchaguzi kutoa matokeo.

Alisema yapo mengi yaliyofanywa na viongozi waliomaliza muda wao na mwaka huu wanatarajia kupata mabadiliko makubwa ya kiutendaji.

Aidha, alisema maendeo hayana chama hivyo aliwasihi wagombea waliokosa nafasi hizo kuacha chuki na badala yake watoe mashirikiano katika kulifikisha mbele gurudumu la maendeleo.

Nae, Mwakilishi mteule wa jimbo la Dimani, Mwanasha Khamis Juma, alisema atahakikisha yale yote aliyoyaahidi katika kampeni zake anayatekeleza.

Alisema ushindi alioupata kwa kupata kura 11,359 ni dhahir kuwa wananchi wa Dimani wamemuamini, ili kuendelea tena kuwaimarishia maendeleo.