WANANCHI wa Zanzibar na watanzania kwa ujumla asubuhi hii wanashuka vituoni kwenda kutekeleza haki ya kikatiba na kidemokrasia ya kuwachagua viongozi.

Kwa upande wa Zanzibar wananchi watapiga kura takriban tano ikiwemo ya  rais wa Jamhuri, watapiga kura ya rais wa Zanzibar, watawachagua wabunge, wawakilishi na madiwani.

Viongozi watakaochaguliwa leo watahudumu kwenye nafasi zao kwa muda wa miaka mitano ambapo jukumu lao kubwa litakuwa kuongoza kwa niaba ya wananchi na kuwatumikia.

Tangu enzi na dahari wananchi wa Zanzibar wakiwemo watumbatu, wapemba, waunguja ni ndugu, ambapo udugu wao hautokani tu kuwa binaadamu, lakini udugu huo unaunganishwa na mambo mbalimbali ya msingi.

Wazanzibari wanaunganishwa na udugu wa damu ambapo kila kona unayopita watu wamechanganya damu, imekuwa shida hivi sasa kuwabagua watu kwa kutumia kigezo cha sehemu waliyotokana.

Ukiachana na mchanganyiko wa damu wazanzibari wengine wamejikuta wakiunganishwa na udugu wa kidini, ambapo mafundisho yanatuelekeza kuwa waislamu wote ni ndugu, hata hivyo, dini hiyo haibagui wala kukataza kuishi vizuri na wasio waislamu.

Si kwamba katika dini hiyo hakuna utofauti wa kifikra, lakini pamoja na hitilafu hiyo waislamu wote wanaabudia mungu mmoja, mtume wao mmoja, kitabu chao kimoja, kibla chao kimoja.

Inashangaza sana wakati kama huu wa uchaguzi mkuu tunasahau misingi inayotuuganisha kama wananchi, tunasahau miongozo inayotuunganisha kama waislamu misingi inayotuunganisha kama binaadamu, misingi inayotuunganisha kama wazanzibari kwa sababu ya siasa.

Kwa kufahamu kuwa hayo yatokea serikali imetuekea sheria kwenye msingi wa uendeshaji siasa na mwenendo mzima wa uchaguzi, lakini tunazikwepa sheria hizo kutokana na baadhi ya hamasa ya viongozi wetu wa kisiasa.

Wakati leo tunaelekea kwenye uchaguzi tungejaribu kila mmoja kadiri awezavyo ahakikishe anadumisha amani kwa maana kwamba jambo lolote atakalolifanya halitamuathiri mwengine.

Hakuna jambo kubwa kwa wakati huu katika nchi yetu kama amani, ambapo kiukweli wapo baadhi ya wanasiasa wanaitishia mambo ambayo yanaweza kuleta machafuko hapa nchini.

Mifano ipo mingi duniani ambapo nchi kadhaa zimeichezea amani ambapo leo wanajjuta kwa yaliyowakuta, katika nchi hizo watu wamepoteza maisha kwa maelefu, wengine wamebakia na majeraha na wengine wakiwa hata hawana makaazi.

Haya yanatokea katika nchi za wenzetu inatupasa yatupe funzo kubwa hasa namna ya kuja kuhangaika na gharama kubwa tutakazokuja zikchukua katika kuirejesha amani tuliyonayo hivi sasa.

Zoezi la kura tulichukulie kikawaida lisitugombanishe, lisisababishe kubaguana, lisitufanye tuchukuane, kwani kufanya hivyo kwa hakika Mwenyezi Mungu hayupo pamoja nasi.

Uchaguzi wa amani Zanzibar inawezekana, piga kura rejea nyumbani hakuna haja ya wewe kuwa chanzo cha kuanzisha vurugu ambazo zitaumiza watu wengine kumbuka dhima kubwa pia utaibeba.

Ewe Mwenyezi Mungu, mola wetu, mola wa viumbe vyote, tujaalie uchaguzi wa salama na amani, wabadilishe wenye nyoyo za kufanya vurugu wawe wahubiri wa amani.