NA HAFSA GOLO

MENEJA wa Narjab Restaurant ya Ziwani Zanzibar, John Matias, amesema atahakikisha anatumia vyema fursa ya kuutangaza utalii wa Zanzibar kupitia tamaduni za vyakula  na vinjwaji vya  asili na vya nje  katika taasisi yake hiyo.

Alieleza hayo mara baada ya tafrija ya uzinduzi wa restaurant hiyo uliofanyika Bomani Unguja alisema  lengo kuu la kuanzisha huduma hiyo ya biashara ni kuisaidia serikali katika kutangaza utalii wa Zanzibar na kuendelea kuwa ni kivutio kwa wageni na wazawa.

Aidha alisema miongoni mwa juhudi atakazozichukua ili kuhakikisha hilo linatimia  ni kufanya kikao cha pamoja  na watembezaji watalii, ili kuona mahitaji ya wageni wanayopendelea ili aweze kuimarisha eneo hilo.

Alisema hatua hiyo itakuwa sambamba na uanzishwaji wa forodhani ndogo katika eneo hilo ambalo litakuwa na haiba na vielelezo ambavyo vitasaidia kutoa historia na tamaduni za Zanzibar kwa wageni.

Sambamba na hilo, alisema anafahamu kwamba changamoto kubwa iliyopo nchini ni suala la upatikanaji wa ajira hivyo atahakikisha anapanua wigo wa kibiashara ili kuongeza idadi ya ajira kwa vijana ikiwemo wazawa.

Nae Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Iddi Shaban Kisauti, alisema dhamira kubwa ya uwekezaji huo ni kuhakikisha anatoa huduma  bora na kuimarisha mazingira bora ya Zanzibar sambamba na kurejesha historia ya kitovu cha biashara.