NA HAJI NASSOR, PEMBA

MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amewataka wanachama wa chama hicho na wananchi kisiwan Pemba, kumpa ridhaa ya kuwa rais, ili aulinde muungano.

Alisema wazanzibar wa leo wanataka mapinduzi mapya ya maendeleo ndani ya Muungano huo, na wa kuyalete hayo sio kiongozi kutoka eneo jengine bali ni yeye Dk. Hussein Ali Mwinyi kupitia chama cha CCM.

Mgombea huyo alisema hayo jana katika uwanja wa Gombani Kongwe alipokuwa akizungumza na wananchi na wanaCCM kwenye mkutano wa ufungaji wa kampeni za kitaifa kwa CCM kwa kisiwani Pemba.

Alisema, muungano huo ni tunu ya taifa na lazima upate rais ambae anaweza kuuenzi na kuundeleza, ambapo kwa Zanzibar ni yeye pakee na kilichobaki ni kwa wananchi kumpa kura akatekelezea kazi hiyo.

“Mimi ndie rais wa kwanza wa Zanzibar, ambae nimezaliwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 pamoja na kuzaliwa kwa muungano, hivyo nna kila sababu ya kuulinda’’,alisema.

Alisema, hayo pia yatanawiri vyema, ikiwa wananchi hao pamoja na wale wa vyama vyengine, watampa ridhaa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli. 

Aidha Dk. Mwinyi alisema moja ya dhamira yake ya kugombea nafasi hiyo, ni kuwatumikia wananchi kwa moyo mmoja na wa dhati, na ndio maana anakusudia kuimrisha huduma za mindombinu ya barabara.

Aliahidi kuwa, miongoni mwa barabara ambazo atazijenga ni ile ya Mkoani- Chake chake, Tundauwa, Wete- Chake chake ambazo hizo ndio zinazounganisha wananchi.

“Lazima suala la ujenzi wa barabara za kisasa liwe jambo la mwanzao, maana hata nia yetu ya kufikisha watalii 850,000 kutoka watalii 6, 0000 wa sasa, wanategemea mno uimarishaji wa miundo mbinu ya barabara,’’alisema.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwinyi alisema atakachokifanya ni kuendeleza pale alipoishia rais wa sasa wa awamu ya saba wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, ambapo anatarajia kuimarisha miundombinu ya afya.

Mapema mgombea mwenza wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan amesema, CCM imewaletea kiongozi mchapakazi kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema sifa za Dk. Mwinyi za nidhamu, uhodari wa kazi, kuwajali watu wote na ubobevu wa uongozi, ambazo hanazo mgombea mwengine yeyote kutoka vyama upinzani.

Alieleza kuwa, Dk. Miwnyi amekuwa anajali sana shida za watu na kupelekea kushika nafasi mbali mbali, kuanzia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‘’Kazi iliyofanywa na CCM na kisha kupatikana kwa mgombea huyo Dk. Hussien Miwnyi haikukosea, maana uchapakazi wake unaonekana na kila anapokabidhiwa madaraka,’’alieleza.

Hata hivyo Mgombea huyo mwenza, alisema Dk. Mwinyi ni muumini mzuri na asieyumba wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964.

“Kama tunatafuta kiongozi ambae anaumwa na Muungano wetu basi huyu Dk. Hussien Mwinyi, kama alivyo mgombea mwanzake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Johan Pombe Magufuli,’’alisema.

Hata hivyo mgombea mwenza huyo ambae pia ni Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amewataka wanaccm na wale wafuasi wa vyama vyengine kuwapigia kura wagombea wote wa CCM.

Aidha alisema kazi iliyofanywa na Dk. Shein, ilikuwa kubwa mno, na ndio maana mwaka 2010 pato lilikuwa wastani wa shilingi bilioni 768, ambapo kwa sasa mwaka 2020 wakati anamalizia muda wake, kuna pato la shilingi tirioni 2.874.

Alisema hata ukusanyaji wa mapato sasa umekua kutoka shilingi bilioni 181 mwaka 2010 ambapo kwa sasa hadi mwaka 2019/2020 kuna makusanyo ya shilingi bilioni 748.9 jambo ambalo ni la kupigiwa mfano.

Kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, alisema una faida kadhaa kwa wazanzibar ikiwa ni moja na kuingia bungeni kwa wabunge kutoka Zanzibar pamoja na nafasi za uteuzi jambo linalowapa haki kuelezea changamoto zao.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Balozi Sief Ali Iddi, alisema jinsi CCM inavyokubalika ushindi wa mwaka huu sio wa kitoto.

Alisema, hilo litawezekana iwapo, wanaccm wote watajitokeza kwa wingi Oktoba 28, mwaka huu kuwapigia kura wagombea wote wa CCM.

Naibu Katibu mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, alisema, ushindi wa CCM hauna shaka, kutokana na kuitekeleza vyema ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.