NA KHAMISUU ABDALLAH

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi, amewataka masheha kuhakikisha wanafanya kazi bega kwa bega na mabalozi wa nyumba 10 ili kutekeleza majukumu yao katika maeneo yao.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akizungumza na mabalozi wa wilaya ya Kusini na wilaya ya Mjini ikiwa ni miongoni mwa kampeni zake za kuzungumza na wananchi na wanaCCM katika mikoa mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Aidha alisema ni jambo la msingi kwa masheha kuwa kitu kimoja na mabalozi kwani hatua hiyo itaongeza usalama wa maeneo yao na kujipanga vizuri kwa kazi zao n ahata kwa chama kwa ujumla.

Alisema, bado mabalozi hawajapata heshima katika jamii hivyo atalifanyia kazi suala hilo ili kuona nao wanajisikia kama viongozi katika maeneo yao.

“Serikali yangu itataka mabalozi washirikishwe katika mambo mbalimbali ambayo hawapati ushirikiano na sio kujulikana wakati wa uchaguzi tu.

Dk. Mwinyi alibainisha kwamba nguzo kuu ya CCM ni balozi wake hivyo aliwahakikishia kuwa serikali ya awamu ya nane inaliweka sawa jambo hilo ili thamani ya kila balozi iweze kutambulika.

Mbali na hayo, aliwaahidi kutafuta njia za kuwapatia maslahi mbalozi ili waweze kufanya kazi zao vizuri zaidi katika kukisimamia chama chao.

“CCM inawategemea sana mabalozi nyinyi kwani ndio mnaofanya kazi katika kutafuta wanachama wa chama chetu,” alisema.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi alibainisha kuwa serikali yake itakikisha inafanya kazi kwa kuwajibika na kuzuia rushwa ili kuona maendeleo ya Zanzibar yanaendelea kubadilika kwa kasi kikubwa kama ilivyofanya serikali ya awamu ya saba chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Mbali na hayo, aliahidi kukutana na mabalozi hao mara kwa mara kwa lengo la kuboresha maslahi yao na chama kwa ujumla. 

Katika hatua nyengine Dk. Mwinyi aliwaagiza kuhakikisha Oktoba 28 kila balozi anahamasisha watu wake wanakwenda kupiga kura.

“Tumezoeleka katika chaguzi nyinyi watu hawapigi kura naagiza zile rasilimali zote zishushwe kwa mabalozi ikiwemo gari na kuona wale wote wakiwemo wagonjwa basi wanapata haki yao ya kupiga kura na CCM tunashida kwa kishindo,” alisema.

Alisema ili CCM iweze kupata ushindi mkubwa ni lazima katika uchaguzi mwaka huu wanaCCM wajitokeze kwa wingi katika zoezi la kupiga kura bila ya kudharau.

Dk. Mwinyi, alisisitiza kwamba amegombea nafasi hiyo kwa dhamira moja ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kuahidi kutowasau mabalozi ambao ndio shina la CCM.

Nao, mabalozi hao walimuomba mgombea huyo atakapoingia madarakani kuwafikiria mabalozi kuwapatia posho ambalo litawasaidia na kuwaingiza mabalozi katika upigaji wa kura za wabunge na wawakilishi kwani wao ndio wanaofanya kazi kubwa katika maeneo yao kutafuta wanachama.

Hata hivyo, waliomba kupatiwa vipande maalum ambavyo vitawawezesha kuwaondolea usumbufu na kutambulika katika maeneo mbalimbali hasa katika maeneo ya ofisi na huduma.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini, Abdalla Mwinyi, alimuahikikishia mgombea huyo mkoa huo umejipanga kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika mkoa huo kuanzia ngazi ya urais, ubunge, uwakilishi na udiwani ili Tanzania iendelee kuwa na heshima hasa ya kudumisha amani na utulivu.