BERLIN,UJERUMANI
UJERUMANI imesema Shirika la Kimataifa la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali (OPCW) limethibitisha kuwa sampuli zilizochukuliwa kwa kiongozi wa upinzani wa Urusi, Alexei Navalny zinaonesha kuwa alipewa sumu.
Msemaji wa Kansela Angela Merkel, Steffen Seibert alisema OPCW ilifanya uchunguzi wake na ilikubaliana na matokeo ambayo tayari yalitolewa katika maabara za Ujerumani, Sweden na Ufaransa.
Duru za OPCW zilieleza kwamba sampuli za damu na mkojo zilionesha kuwa na kemikali ya “cholinesterase inhibitor” ambayo ni sawa na sumu ya Novichok inayoathiri mishipa ya fahamu.
Seibert alisema uchunguzi huo unathibitisha kwa mara nyengine tena kwamba Navalny alikuwa mwathirika wa shambulizi la kemikali ya Novichok.
Seibert alisema Ujerumani inaendelea kuitaka Urusi kuchunguza kikamilifu na kueleza kile kilichotokea kwa Navalny na kwamba itajadiliana kuhusu hatua zinazofuata na Baraza Kuu la OPCW pamoja na washirika wake wa Umoja wa Ulaya.