LONDON, England

MESUT Ozil, nyota wa klabu ya Arsenal inaelezwa kuwa amepewa mkataba wa miaka miwili kusaini ndani ya klabu ya Al-Nassri ya barani Asia ikiwa kiungo huyo atakubali.

Kiungo huyo hajacheza kikosi cha Arsenal chini ya kocha Mkuu, Mikel Arteta tangu Machi 7, jambo linalomaanisha kwamba sio chaguo la kwanza la kocha huyo.

Ripoti zinaeleza kuwa Ozil mwenye miaka 31 ameambiwa afanye chaguo la kuondoka ndani ya kikosi hicho ili kupata changamoto mpya kutokana na kukosa namba kikosi cha kwanza.

Mpango huo unaonekana kuwa mgumu kwa kuwa mchezaji mwenyewe ameweka wazi kuwa anaipenda Arsenal na furaha yake itadumu ikiwa atabaki ndani ya kikosi hicho licha ya kwamba hana nafasi ya kucheza.

“Mambo yamekuwa magumu kwangu hilo ninajua lakini ninaipenda Arsenal, nimeamua kuwa bado nina nafasi ya kufanya vizuri hali ambayo ninakutana nayo kwa sasa ni sehemu ya kunifanya niwe imara zaidi,” amesema Ozil.