LONDON, England
KIUNGO wa Ujerumani, Mesut Ozil, hatakuwepo kwenye kikosi cha Arsenal kwa ajili ya Ligi ya Europa.

Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 31 hajaichezea Arsenal tangu Machi mwaka huu na hatma yake klabuni hapo imekuwa mashakani kwa muda mrefu .
Ozil ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa katika historia ya Arsenal na hajaonekana tangu kwa miezi kadhaa.

Alipoulizwa hivi karibuni kwanini mshindi huyo wa Kombe la Dunia alikuwa amepoteza nafasi, kocha Mikel Arteta alijibu: “Timu inabadilika, unaweza kuona kiwango wanachofikia . “Hapa ndipo tulipo kwa sasa. Tunataka kubadilika zaidi na kucheza vizuri na kushindana vizuri.

“Tunahitaji kuendelea kudumisha hali hiyo. Nina furaha na utendaji hapa, kwa kinachoonyeshwa na wachezaji inaniwia ugumu kuchagua kikosi pia si rahisi Ozil kupata nafasi”.

Siku ya Jumanne, Ozil alijitolea kulipa mshahara kamili wa Jerry Quy ambaye anavaa kinyago kinachohamasisha mashabiki wa washika bunduki hao kwa miaka 27 iliyopita na hivi karibuni alitangaziwa kusitishiwa huduma yake kutokana na kuporomoka kiuchumi kwa klabu hiyo.
Kampeni ya Ligi ya Europa ya Arsenal itaanza wakati watakapomenyana na wapinzani wa kundi ‘B’, Rapid Vienna huko Austria mnamo Oktoba 22 kabla ya mechi dhidi ya Dundalk na Molde.(Goal).