NA MWAJUMA JUMA

WANANCHI wa kijiji cha Donge Shehia ya Pale Mkoa wa Kaskazini Unguja,  wametakiwa kuendelea kudhibiti vitendo vya udhalilishaji, ili visitokee kwenye shehia yao.

Akizungumza  wakati wa utoaji elimu ya udhalilishaji kwa wananchi hao Ofisa Ustawi wa jamii, Makame Makame Haji, amesema kwa mwaka 2019/2020 katika shehia ya Pale, hakuna kesi za udhalilishaji zilizoripotiwa kwenye vyombo vya sheria si Polisi wala Mahakamani.

Alisema kuwa pamoja na kuwa vitendo hivyo havijafanyika lakini wana wajibu wa kuongeza nguvu ya mashirikiano ya kuwalinda watoto wao, ili wasijewakafanyiwa.

Makame aliwataka wananchi hao kuendeleza msimamo wao wa kuvipiga vita vitendo  hivyo,  ili  kijiji hicho kisiingie  katika historia mbaya  kuwa na kesi za udhalilishaji wa watoto.

Kwa upande wao  baadhi ya watoto waliopatiwa elimu ya udhalilishaji wamewaambiwa Maafisa wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto pamoja na Mratibu wa SOS kuwa vitendo wanavyo fanyiwa zaidi ni kupigwa wakiwa Majumbani, Skuli na chuoni jambo linalowakosesha furaha na amani.

Hivyo  watoto hao, waliiomba Serikali  kuendelea kupiga vita upigwaji wa mikwaju,   kwani bado unaendelea katika skuli  na  majumbani badala yake kutafute adhabu mbadala kwa watoto kupewa pale wanapofanya makosa na sikupigwa fimbo.