WASHINGTON,MAREKANI

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amekosolewa vikali na makasisi wahafidhina wa kanisa hilo, kutokana na kauli yake inayoashiria kuwa anaunga mkono mahusiano na ndoa za watu wenye jinsia moja.

Mmoja wa viongozi wa Katoliki waliomjia juu Papa ni Askofu Thomas Tobin wa Providence, makao makuu ya jimbo la Rhode Island la Marekani .

Alisema bayana kuwa taarifa ya Papa inapingana wazi wazi na mafundisho na msimamo wa muda mrefu wa Kanisa Katoliki juu ya mahusiano ya watu wenye jinsia moja.

Askofu Tobin alisisitiza kuwa, kamwe kanisa hilo halitaruhusu au kubariki uozo wa namna hiyo wa kijamii.

Katika makala iliyorushwa hewani na Tamasha la Filamu la Rome, Papa alionekana kuunga mkono ndoa za watu wa jinsia moja kwa kusema, mabaradhuli wana haki ya kuwa katika familia, wao ni watoto wa Mungu.

“Huwezi kumfukuza mtu katika familia au kuyafanya maisha yake yawe mabaya kutokana na hili,”alisema.

Katika makala hiyo, Papa alisema kinachopaswa kufanywa ni kuundwa sheria za kuwalinda watu walioko au wanaotaka kujiingiza katika mahusiano hayo ya watu wa jinsia moja.

Mapema mwaka huu, Kiongozi wa zamani wa Kanisa Katoliki Duniani Benedict XVI alimtaka Papa Francis kusitisha mpango wa Kanisa Katoliki wa kuruhusu wachungaji wenye wake kuwa makasisi na maaskofu wa kanisa hilo, mpango ambao Papa Francis anauunga mkono kutokana na kile kinachosemekana kuwa ni kupungua idadi ya viongozi wa kidini katika baadhi ya maeneo ya dunia kwa sababu ya kubanwa na sheria ya kutoruhusiwa kuoa.