LONDON, England
KIUNGO wa kimataifa wa Manchester United na Ufaransa, Paul Pogba, amekiri kwamba ni ndoto yake kuichezea Real Madrid siku moja.

Lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 aliongezea kwamba atatumia kila njia kuiweka United pale inapotaka kuwa msimu huu kwa mafanikio.

Kiungo huyo amekuwa akihusishwa na uhamisho wa kuondoka Old Trafford ambako alijiunga nayo kwa mara ya pili kwa dau la pauni milioni 89 mwaka 2016.Kandarasi ya mshindi huyo wa Kombe la Dunia inaisha msimu ujao.

Ijapokuwa United ina haki ya kumuongezea kandarasi ya mwaka mmoja. Pogba amesema kwamba hajakuwa na mazungumzo yoyote na klabu hiyo kuhusu kuongeza kandarasi yake.
“Hakuna mtu aliyeniambia chochote”, alisema katika mkutano na wanahabari akiwa na kikosi cha timu ya Ufaransa juzi.

“Sijazungumza na Ofisa Mkuu Mtendaji, Ed Woodward, hatujazungumza kuhusu mkataba mpya”.
“Kwa sasa niko katika klabu ya United na najaribu kuimarisha mchezo wangu. Najua kuna wakati ambapo klabu itanifuata na kuzungumza nami na pengine kuniwasilishia ombi fulani au laa”.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kujiunga na Real Madrid ambayo amekuwa akihusishwa nayo, alijibu: “Wachezaji wote wangependelea kuichezea Real Madrid , ni ndoto yangu, kwanini siku moja nisijiunge nao?.

“Nipo United na naipenda klabu yangu, naichezea United, na nataka kuiweka inapohitajika kuwepo”.
United imeanza vibaya ligi msimu huu ikishinda mara moja katika mechi tatu.
Pogba ameanzishwa katika mechi zote msimu huu baada ya kujitenga alipoambukizwa virusi vya ‘corona’ mwezi Agosti.(Goal).