WARSAW POLAND 

WAPIGA mbizi wa jeshi la Poland wameanza operesheni ya hatari ya kunasua bomu kubwa la Uingereza lililotumika kwenye vita vya pili vya dunia lililo chini ya bahari.

Takribani wakazi 750 wameondolewa kutoka kwenye eneo hilo, lililo karibu na mji wa bandari wa Swinoujscie, ambapo operesheni hiyo inatarajiwa kuchukua siku 5.

Bomu liitwalo Tallboy, au bomu la ”tetemeko la ardhi” lina urefu wa mita 6 na uzito wa tani 5.4.

Bomu hilo lilidondoshwa wakati wa uvamizi mwaka 1945 ambapo tukio hilo lilizamisha meli ya Ujerumani ya Lützow, ambapo lipo chini ya bahari umbali wa mita 12 na kinachoonekana juu sehemu ya pua ya bomu hilo.

Kazi iliyopo sasa ni kuhakikisha bomu hilo linaondolewa kwa kutumia chombo maalumu kutoka mbali, na wapiga mbizi tayari wameliandaa eneo hilo kwa siku kadhaa.

Poland haijawahi kunasua bomu kubwa kama hilo chini ya maji hapo kabla na kwamba bomu la Tallboy linalosababisha mtetemeko linaporipuka.

Majeshi ya anga ya Uingereza yaliangusha mabomu ya aina hiyo mwaka 1944-45 kwa kutumia ‘Lancaster bombers’ na maeneo ya kurushia roketi ya jeshi la Ujerumani Nazi – V yalikua miongoni mwa maeneo yaliyokuwa yakilengwa.