NA ASIA MWALIM

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja  (ACP) Awadh Juma Haji, amesema wameanzisha uchunguzi wa kubaini chanzo cha kunasa kwenye umeme Mama na Mwanawe.

Aliyasema hayo akizungumza na Zanzibar Leo, ofisini kwake Mwembemadema Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja,  ambapo alisema wameanzisha uchunguzi huo baada ya tukio hilo lililotokea Oktoba 2, mwaka huu, saa 2:00 za asubuhi.

Kamanda huyo aliwaja watu hao ni Mtumwa Abdallah Maulid (36) na Fatma Rajab  Kesi (17) wote ni wakaazi wa Fuoni Kipungani Unguja, ambao ni mama na mwana.

Alisema chanzo cha tukio hilo wamebaini lilitokea baada ya Mtoto huyo kugusa waya wa fensi ya nyumba ya jirani uliokatika na alipougusa alianza kupapatika kusababisha kunasa na wakati Mama yake akimnasua na yeye alinasa na kupoteza fahamu.

Aidha Kamanda alisema wakati tukio hilo likiendelea kwa bahati nzuri alitokea jirani yao na kwenda kutoa (cut-out) ambapo umeme ulizima na kupelekea kuwaokoa wote wawili,.

Kamanda alisema wawili hao, baada ya tukio walipelekwa katika Hospitali ya KMKM Kibweni, ambako wamelazwa na wanaendelea kupatiwa matibabu.

Hata hivyo, Kamanda aliwataka watu wanaotumia vifaa vya umeme kudhibiti vizuri ili kuepusha ajali za umeme, kwani madhara yake ni makubwa, sambamba na kuiomba jamii kuwa na tahadhari juu ya matumizi ya nishati hiyo.