NA MWANDISHI WETU

KAMANDA wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji, amewataka wananchi leo kujitokeza vituoni kupiga kura kwani wamefanikiwa kudhibiti fujo zilizopangwa kufanyika jana katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari, mjini Unguja jana, wakati akiwa kwenye operesheni ya kuweka mji katika hali ya usalama, wakati wa zoezi la kupiga kura ya mapema iliyoendeshwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kamanda Awadh, alisema jeshi la Polisi limefanikiwa kudhibiti fujo hizo baada ya kuwakamata watu waliojaribu kutaka kuharibu mali na kwa kuweka mawe barabarani huku wakiwasha maringi ya moto.

Alisema maeneo ambayo yalifanyika fujo hizo ni pamoja na Kinuni, Garagara na Magogoni, ambapo watu walioendesha fujo hizo wamekamatwa na watachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na askari wa vikosi vyengine vya ulinzi na usalama wamefanyakazi zao vizuri na kudhibiti vitendo hivyo ili visilete madhara kwa jamii.

“Wananchi wanatakiwa kujitokeza bila ya kuwa na hofu kwani tumejipanga kuwadhibiti wale wote waliojipanga kufanya fujo na uvunjifu wa amani kwa lengo la kuwatisha,” alieleza.

Kuhusu kukamatwa kwa mgombea wa urais wa chama cha ACT- Wazalendo, Seif Sharif Hamad, aliyedaiwa kufika katika kituo cha kupiga kura cha Mtoni Garagara, Kamanda alisema hadi wakati huo hakuwa na taarifa hiyo.

“Sina taarifa na hilo jambo kwani toka asubuhi nimekuwa katika operesheni na vijana wangu kudhibiti fujo mitaani hivyo siwezi kuzungumzia jambo ambalo sina taarifa nalo,” alieleza kamanda Awadh.

Taarifa zinaeleza kwamba, Maalim Seif alifika katika kituo hicho majira ya asubuhi kwa lengo la kupiga kura, lakini aliondolewa na maofisa usalama baada ya msimamizi wa uchaguzi wa kituo hicho kumueleza kuwa hakuwa katika orodha ya watu wanaopaswa kushiriki uchaguzi huo kwa jana.

Hata hivyo majira ya mchana mgombea huyo alishuhudiwa na Zanzibar Leo katika kituo cha kupigia kura cha Mwembeshauri akitembelea kukagua mwenendo wa uchaguzi huo hali inayopingana na uvumi kwamba kiongozi huyo kuwa alikamatwa na kushikiliwa na vyombo vya dola.