NA TATU MAKAME

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, limewatahadharisha vijana kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani katika kipindi hiki wananchi wanapokwenda kushiriki zoezi la upigaji wa kura.

Hata hivyo, aliwatanabahisha vijana kutoshiriki zoezi la uchaguzi Oktoba 27, ikiwa hawakuomba kushiriki zoezi hilo kwa siku hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja,Kamishna Msaidizi wa Polisi, Haji Abdalla Haji, alisema siku hiyo watakaoshiriki zoezi hilo ni wale watu maalum ambao wako kisheria.

Alisema Tume ya uchaguzi imewaruhusu watu maalum kupiga kura siku ya Oktoba 27 kwa mujibu wa sheria namba 4 ya mwaka 2018 sheria ya uchaguzi kifungu cha 82 (2) (a) (b).

Alifahamisha kuwa kwa mujibu wa kifungu hicho wapo watu ambao watashiriki zoezi hilo ambao waliruhusiwa na tume vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kama Polisi na watu wengine hivyo atakaekwenda kushiriki zoezi hilo kabla ya Oktoba 28, atachukuliwa hatua za kisheria.

“Mtu atakaekwenda kupiga kura bila ya kuwa na sababu maalum au ruhusa ya tume hatutomuachia kwani atakuwa anaharibu uchaguzi, sisi kama jeshi la Polisi tumejipangam kwa hilo,alisema Kamanda Haji.

Alitumia nafasi hiyo kuwa watendaji wa jeshi la polisi tayari wamepewa mafunzo ya kutosha ya kusimamia zoezi la upigaji wa kura na atakaejaribu kwenda kwenye vituo vya kupigia kura au kuharibu atawajibishwa.

Kamanda huyo aliwataka wazazi kutowaachia watoto kwenda maeneo ya mbali na makaazi yao ili kuongeza usalama wao.