NA ASYA HASSAN

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, limesema linaendelea kuwasaka watu waliyohusika na tukio la kuwachoma sindano watoto watatu.

Akizungumza na gazeti hili Kamanda wa Polisi Mkoa huo Kamishina msaidizi wa Polisi, Awadhi Juma Haji, alisema jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo pamoja na kuwatafuta watu hao, ili waweze kuwachukulia hatua za kisheria.

Alisema licha ya serikali na taasisi mbalimbali kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa watoto, wapo baadhi ya watu wanatafuta mbinu nyengine kuwadhalilisha watoto hao ili waweze kuvuruga mfumo wa maisha yao.

Aidha alisema hawafahamu lengo na dhamira ya watu hao kufanya matukio hayo, lakini wachoamini ni njia mojawapo ya kuendeleza vitendo viovu hapa nchini, hivyo jeshi hilo limejipanga kuimarisha ulinzi na usalama, ili kuweza kudhibiti matukio yote ya kihalifu.

Kamanda huyo alisema jeshi hilo halipotayari kuona vitendo hivyo vikiendelea kutokea kwa jamii, hivyo watahakikisha wanashirikiana na vituo vya polisi vya Mikoa tofauti, ili waweze kufanikisha kupatikana kwa wahusika hao.

Sambamba na hayo, Kamanda Awadhi, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuwa tayari kushirikiana na jeshi hilo kwa kuwafichua watu hao, ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mbali na hayo aliwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao, ili waweze kuwanusuru na matukio tofauti ya kihalifu ambayo yataweza kuvuruga mfumo mzima wa maisha yao.