NAIROBI,KENYA

RAIS wa Kenya Uhuru Kenyatta ameliongoza taifa katika maadhimisho ya siku ya Mashujaa kwa kutoa wito wa kuwepo makubaliano ya katiba ambayo itahudumia jamii zote na kusisitiza usawa na umoja wa kitaifa pamoja na tahadhari aliyoitoa dhidi ya ugumu ambao huzaa siasa hasi na zinazogawanya.

Alifafanua kuwa viongozi waasisi na mashujaa wa katiba hawakuwa na nia ya kufanya utaratibu wa katiba uwatumikishe bali waliiunda katiba hiyo ili iwatumikie wao, na endapo itashindwa kuwatumikia wanaweza kuangalia mfano wa waasisi wao na kufikiria tena upya.

Kauli hii ya rais ilikuja wakati mjadala wa kama katiba ya mwaka 2010 ifanyiwe marekebisho au la ukizidi kupamba moto nchini Kenya, ambao umechochewa na Mpango wa Ujenzi wa Madaraja BBI, mradi ambao unalenga kukuza umoja wa kitaifa ulioanzishwa na Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.