BISHKEK, KYRGYZSTAN

RAIS Soornbai Jennbekov wa Kyrgyzstan ametangaza kujiuzulu kufuatia maandamano ya umma dhidi ya uchaguzi wa bunge uliovipa ushindi vyama vinavyomuunga mkono.

Hatua hiyo iliyotangazwa jana, inayomfanya Jennbekov kuwa kiongozi wa tatu kuangushwa na maandamano ya umma, ndani ya kipindi cha miaka 15, katika taifa hilo la Asia ya Kati.

Wafuasi wa hasimu wake, Waziri Mkuu mpya Sadyr Zhaparov, waliingia tena mitaani hapo jana, na kutishia kuyachoma moto majengo ya serikali, ikiwa kiongozi wao huyo hakutangazwa, kukaimu nafasi ya urais.

Katiba ya Kyrgyzstan inamtaka spika wa bunge kuchukuwa madaraka, pale Rais anapoondoka, lakini kwa mujibu wa Zhaparov, Spika huyo amekataa kuongoza serikali ya mpito.

Zhaparov, ambaye alikuwa amewekwa kizuizini kabla ya kuachiliwa huru na waandamanaji wiki mbili zilizopita, aliwaambia wafuasi wake kwamba madaraka yote ya uwaziri mkuu na urais, sasa yamo mikononi mwake.