NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamhuri ya Malawi, Dk. Lazarus McCarthy Chakwera anatarajiwa kuwasili leo nchini kwa ziara ya siku tatu ya kitaifa ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi mbili hizo na kuendelea kudumisha ujirani mwema.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amesema akiwasili nchini atapokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Alisema Dk. Chakwera itakuwa ziara yake ya kwanza kuja kutembelea Tanzania baada ya kuingia madarakani mwezi Juni mwaka huu, ambapo kabla ya hapo alitembelea nchi za Zambia na Zimbabwe.

Alisema baada ya kuwasili nchini Rais huyo atapata fursa ya kutembelea bandari ya Dar es Salaam, kituo cha kuhifadhia mizigo cha Malawi ambacho kimekuwa alama muhimu ya mashirikiano kati ya Tanzania na Malawi, kilichopo bandarini hapo.

Wakati huohuo Rais Chakwera akiwa na mwenyeji wake, Dk. John Pombe Magufuli wataweka jiwe la msingi katika kituo cha mabasi ya kwenda mikoani Mbezi mwisho, ikiwa ni ishara ya mashirikiano ya umoja katika uendelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aidha alisema nchi hizo mbili zimeendelea kushirikiana katika ziara, nyanja za kisiasa, ulinzi na usalama, kiuchumi kijamii na ya kikanda hususani ndani ya jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) na umoja wa Afrika.

Alieleza kuwa nchi ya Malawi ni miongoni mwa nchi zenye uwekezaji hapa nchini, ambapo umejikita katika sekta mbalimbali zikiwemo fedha, uzalishaji, usafirishaji, ujenzi, kilimo na mafuta.

Alifafanua takwimu za kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) za mwezi Septemba mwaka huu zinaonyesha kuna jumla ya miradi minane kutoka Malawi ambayo ina jumla ya thamani ya dola milioni 30.1.

Alieleza kuhusu mashirikiano ya biashara kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) zinaonyesha kwamba kiwango cha bidhaa ambazo Tanzania imesafirisha kwenda Malawi kimezidi kuongezeka kutoka shilingi blioni 111,082.70 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 130,758,10m kwa mwaka jana.