GITEGA,BURUNDI
RAIS wa zamani wa Burundi,Pierre Buyoya amesema kuwa amekataa hukumu ya kifungo cha maisha jela aliyopewa bila kuwa Mahakamani wiki hii kuhusiana na mauaji ya mwaka wa 1993 ya mtangulizi wake.
Buyoya aliipuuza kesi hiyo akisema ilichochewa kisiasa na alihukumiwa na mahakama moja nchini Burundi kwa shambulizi dhidi ya kiongozi wa taifa kuhusu kuhusika kwake katika mauaji ya rais Melchoir Ndadaye mwaka wa 1993.
Buyoya ambaye kwa sasa ni mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali alisema katika taarifa yake kuwa hukumu hizo za mahakama haziwafunganishi kisheria.
Buyoya ambaye ni Mtutsi, aliingia madarakani kwa mara ya kwanza katika mapinduzi ya mwaka wa 1987, lakini akajiuzulu baada ya kushindwa katika uchaguzi na Ndadaye.
Ndadaye, kisha akawa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia 1993, lakini miezi minne tu baada ya kuapishwa akauawa na wanajeshi wa Kitutsi.
Mauaji yake yaliitumbukiza nchi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.