Matarajio yake ni kuanzisha chuo kitakachoitangaza Z’bar
ZASPOTI

KATIKA mizunguko yangu ya kawaida nilifika katika uwanja wa ndege wa kimataifa Zanzibar wa Sheikh Abeid Amani Karume mara baada ya kufika hapo nilitembelea kwenye mkahawa mmoja unaojulikana kwa jina la Zenji Cafe.


Katika mkahawa huo niliona niliona mlango ambao kwa jina la umaarufu ‘Zanzibar Door’ ambapo nilitaka kupita kwa bahati wafanyakazi wa mhakawa huo waliniwahi na kunambia kwamba hiyo ni picha na sio mlango wenyewe.


Kusogea mbele katika mkahawa huo wa Zenji Cafe nilikutana na picha ya bibi na bwana akiwa anaweka kahawa katika kikombe na kahawa,picha ambayo imechorwa kwa ustadi mkubwa sana.
Kwa kweli bada ya kuona picha hizo zilizonivutia mimi pamoja na wageni ambao walifika katika mkahawa huo na wengine waliweza kupiga picha kwa ajili ya kumbukumbu ya sehemu hiyo.


Kutokana na kuvutiwa na picha hizo ilinilazimu niulize aliechora picha hizo ni nani na niliambiwa na kufahamishwa katika ofisi yake na kunifanya niache kazi na nifunge safari mpaka katika ofisi ya uchoraji inayojulikana kwa jina la ‘Zanzibar Art Studio’ iliopo katika maeneo ya Forodhani.
Baada ya kufika hapo nilimuulizia na baadae kumuona na nilimueleza nilichokifuata kwake hakukataa alinipa mashirikiano makubwa alipoanzia,alipofikia na matumaini yake ya hapo baadae.


Kwa umbile la nje Ramadhan Awesu ni kijana mfupi mwenye rangi ya maji ya kunde mcheshi na mpenda masihara ambapo katika mazungumzo yetu yaliingiliana na utani ulionogesha mahojiano hayo.
Kama ilivyo desturi ya muumini wa dini ya kiislamu,kijana huyo alianza kujifunza elimu ya dini ikiwemo kitabu kitukufu cha Quraan pamoja na vitabu vyengine vikiwemo vya hadithi za kiongozi mkuu wa waislamu, Mtume Muhammad (SAW),Fiqhi na Sira .


Awesu alizaliwa Agosti 13 mwaka 1989 katika hospitali ya Temeke iliyopo kwenye wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam,ambapo elimu yake alisema alianzia visiwani Zanzibar katika skuli ya Darajani mwaka 1996 na kumaliza elimu ya msingi mwaka 2002.
Baadae aliendelea na elimu ya sekondari katika skuli ya Vikokotoni mwaka 2003 na baadae kujiunga na skuli ya Lumumba alipomaliza kidato cha nne mwaka 2007 na hakuendelea tena na masomo ya skuli.


“Kwa kweli baada ya kumaliza kidato cha nne sikuendelea tena na masomo ya skuli kutokana na sikua na alama nzuri katika masomo yangu hayo na nikaingia katika fani nyengine .
Alisema baadae alijiunga na elimu nyengine ikiwemo kutembeza wageni,udereva,upishi, mchezo wa karate pamoja na masomo ya uchoraji ambayo ndio kazi alioiendeleza katika masomo aliojifunza.


Rama alisema mbali ya kujifunza fani nyingi lakini fani hiyo ya uchoraji ndio alioipenda kutokana an kuwepo ndani ya damu yake kwa sababu ndugu zake wengi walikuwa wachoraji ingawa hawakuendelea na fani hiyo.


“Kwa kweli nilipokuwa najifundisha mchezo wa karate mwalimu wangu mmoja ndie aliegundua kipaji changu cha uchoraji kwa sababu miongoni mwa masomo ya mchezo huo ni mbinu za kujilinda, tulikua tukifundishwa kwa kutumia michoro ,yeye alinisaidia kunikutanisha na walimu wa sanaa hiyo wakaanza kunifundisha na ndio safari yangu ikaanzia hapo,”alisema.


Alisema kwamba akiwa katika kujifunza kazi hiyo alikutana wachoraji wengi mahiri aliowataja kwa majina akiwemo Seif Soud,Said Ramadhan,Suleiman Rashid ‘Binda’,Medi na wengine wengi ambao wote kwa pamoja walikuwa wakimsaidia kufanikisha ndoto zake zinatimia.
Mwaka 2001 Ramadhan alianza kuchora picha yake ya mwanzo wakati huo alisema akiwa mwanafunzi wa skuli akiwa darasa la sita ambayo ilikua inamuonesha babu anashona kofia ya mkono.


“Nakumbuka picha yangu ya mwanzo kuchora ilikua babu anashona kofia ya mkono picha ilikua nzuri sana na iluzwa kwa sarafu ya dola za Kimarekani ilikua dola 70,”alisema.
Baada ya hapo Rama alisema aliendelea na fani hiyo mpaka hivi sasa na ndio kazi inayompatia riziki ya kula yeye na familia yake.


Mchoraji huyo ambae anachora picha za aina mbali mbali zikiwemo za katuni,za sura za watu,za makampuni, vitabu anasema taangu kujiunga na fani yake hiyo hajaona tatizo lolote linalomkabili zaidi ya watu baadhi ya watu kudharau kazi hiyo.


“Tangu nimeanza kazi hii sijaoa tatizo lolote nilokutana nalo zaidi ya baadhi ya watu kunidharau na kuona hii kazi haina maana lakini kwa upande wa faida Alhamdulilah nimeoa, nimenunua usafiri, nimenunua kiwanja, na pia nimeweza kufahamiana na watu wa mataifa mbalimbali,”.


Nilipomuuliza kuhusu wateja wanaonunua picha hizo ni wazalendo alisema kwamba wachache sana wazalendo na wateja wao wakubwa ni kutoka mataifa ya nje hususan wazungu na waarabu.
Kuhusu kuvutiwa na wachoraji wengi kijana huyo alisema anavutiwa na wachoraji mbali mbali kwani kila mchoraji wa picha ana utaalamu wake,hivyo aanaemuona anachora uzuri humvutia.
Ramadhan alisema zile picha alizochora pale katika mkahawa uliopo kwenye uwanja wa ndege ya Abeid Amani Karume alipata tenda na zimeweza kumpatia umaarufu kutoka na ubora na hadhi ya picha hizo .


Mchoraji huyo alisema matarajio yake ya baadae kuweza kumiliki eneo lake la uchoraji ambalo litaweza kuzalisha wachoraji mahiri watakaoitangaza vyema Zanzibar katika ramani ya dunia.
“Matarajio yangu ya baadae kuweza kumiliki eneo langu mwenyewe ambalo litakua kama ni chuo kitakachotoa wachoraji wengi na wazuri katika fani hiyo ili waweze kujiajiri na kuitangaza nchi yetu kupitia kazi yao hiyo,”alisema


Msanii alitoa ushauri kwa jamii kutambua na kuthamini kazi zinazofanywa na wasanii wa uchoraji kwani wao pia ni sehemu ya jamii na sehemu ya ajira kama walivyo waajiriwa wa serikalini.
Alisema sio vyema kuona watu wakaona wachoraji ni watu ambao hawana maana katika jamii na kuwadharau wakati wao pia wanategemewa katika familia zao na kufanya mambo ya muhimu.


Kwa upande wa serikali, aliishauri wizara husika kutambua mchango wa wachoraji katika katika kusukuma gurudumu la sanaa pamoja na kwa kutoa fursa kwa wachoraji kuwapatia mafunzo zaidi.
“Naiomba Serikali kupitia wizara yetu kutusaidia na sisi wasanii wa uchoraji kwa kutambua mchango wetu kwa kutusaidia katika kujifunza zaidi pamoja na kututafutia nafasi za kwenda nje kwa ajili ya maonyesho ya kama wanavyofanya kwa waigizaji na wanamuziki,”alifafanua.


Ramadhan Awesu amefanikiwa kuoa na kujaaliwa kupata watoto, hivi sasa wamesimama kufanya kazi hiyo kutokana na kutokuwepo kwa wanunuzi wa bidhaa hiyo ambao wamesita kufika nchi kwa kuzuka maradhi ya ‘corona’.