GASPARY CHARLES-PEMBA

REDIO Jamii Micheweni imefanikiwa  zaidi katika uzalishaji wa maudhui bora ya vipindi vya redio licha ya kukabiliwa na changamoto  ya uwezo wa kifedha.

Meneja wa redio hiyo, Ali Masoud Kombo  alisema , ni furaha kuona mafaniko yote yanatokana na uwezo waliojengewa na mashirika mbalimbali, likiwemo Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Redio hiyo iliongoza nchini Tanzania mwaka 2019 kwa ubora wa maudhui ya Redio katika utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar- es- Salaam, ambapo mashirika hayo yaliiwezesha kiutaalamu na kiutawala.

Alieleza  kupitia mpango mkakati ulioandaliwa, kituo kiliweza kupata wadau wapya wa kushirikiana na kufanya nao kazi ambao ni (TAMWA Zanzibar), ActionAid, na RTI ambapo kupitia wadau hao imesaidia kuongeza mapato ya kituo kwa kiwango cha shilingi milioni 11.

Alisema ujuzi wa ufuatiliaji na tathmini umekipa nguvu kituo hicho kukusanya taarifa kwa wakati kutoka kwenye vipindi vyake na kuziweka kwenye kumbukumbu kwa ajili ya kuzishirikisha kwa wadau wengine, kuzichambua pamoja na kujibu maswala yaliyojitokeza iwe ya ndani au nje.

Aliongeza kuwa kituo hicho pia kimeimarisha utumiaji wa teknolojia kwa kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii ikiwamo Facebook, Twitter na Instagram ambayo inasikika hadi nje ya  mipaka ya  eneo la redio jamii ya Micheweni.

Meneja huyo, alisema kuwa changamoto pekee ambayo kituo kinakabiliwa nayo kwasasa ni ukosefu wa fedha za kutekeleza mipango yake kabambe ambayo inahusu kuandika na kufuatilia maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyofikiwa na jamii ya Micheweni sambamba na kubaini changamoto zilizojitokeza.