WANANCHI wa Kijiji cha Muzi, Kata ya Kasanga, Wilayani Kalambo Mkoani Rukwa wameelezea hisia zao juu ya faida za kuanza kufanya kazi kwa kiwanda cha samaki cha Alpha Tanganyika Flavour

Kituo chake cha kukusanyia samaki katika Kijiji hicho kuwa kitakuwa mkombozi kwa wavuvi wengi baada ya wavuvi hao kuendelea kupata hasara kutokana na samaki wao kukosa soko la uhakika.

Mmoja wa wavuvi wa Kijiji hicho, Malona Sichilima, alieleza kuwa wakati kiwanda hicho kilipokuwa kinafanya kazi wavuvi walikuwa wanauza samaki wao kwa bei nzuri Zaidi tofauti na hali ilivyo sasa ambapo wavuvi wanawauzia wachuuzi samaki kwa bei ya hasara na matokeo yake kudumaza maendeleo yao.

“Tunashukuru sana mwekezaji kuja Kijiji cha Muzi, kuja kuwekeza ili na sisi wavuvi tupate faida kile kipindi tulikuwa tunavua samaki tunawauzi wachuuzi sanduku moja shilingi 50,000/= ila kipindi cha nyuma kwenye kiwanda tulikuwa tunauza shilingi 100,000/= hadi 150,000/= hivyo yunamuomba mwekezaji huyu atupangie bei nzuri,” alisema.

Halikadhalika, Baraka Kafue, ambaye naye pia ni mvuvi katika Kijiji hicho alisema kuwa kwa muda mrefu wavuvi wa mwambao wa ziwa Tanganyika wamekosa soko la kuwaingizia faida kutokana na biashara hiyo ya uuzaji wa samaki na hivyo kumshukuru mwekezaji huyo mwenye nia ya kukifanya kiwanda kianze kufanya kazi.

“Tunashukuru kwa kutuletea fursa ya kufungua kiwanda tena kwa mara nyingine, kwasababu tumepoteza soko la kuvua samaki, tumekuwa tukivua samaki, lakini tunakosa kwa kuuza na tukiuza tunauza kwa bei ya hasara yaani kutoka samaki 10 kwa 2,000/= hadi samaki 20 kwa 2,000/= maana yake inatupunguzia kipato maana yake ukiwa na samaki 100 unapata 20,000/= badala ya kupata 40,000/= hivyo kiwanda kikifunguliwa kitatusaidia sana,” Alisema