NA ZAINAB ATUPAE

TIMU ya Ruvu Shooting imeondoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Jang’ombe Boys, ikiwa mchezo wa kirafiki ulioandaliwa na timu ya Jango’mbe boys kwa lengo la kuadhimisha wiki ya Jang’ombe.

Mchezo huo uliotimua vumbi uwanja wa Mao Zedong  ‘A’ majira ya saa 10:00 jioni,ulikuwa na mashabiki wengi na kuvutia kwa muda wote.

Pambano hilo lilikuwa na ushindani ambapo timu zote ziliingia uwanjani zikiwa na mbwembwe,huku kila mmoja akijiamini kuwa ataondoka na ushindi.

 Ruvu ilianza kuandika bao la kwanza mapema kipindi cha kwanza kwenye dakika ya saba lililofungwa na David Richard.

Hata hivyo bao hilo halikuwavunja moyo Jang’ombe boys na walijipnga upya kujibu mashambulizi kutafuta bao la kusawazisha, ambapo walifanikiwa kupata bao hilo dakika 21 lililofungwa na Ali Rashid Othman, mabao ambayo yalidumu hadi daika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika.

 Kurudi uwanjani kumalizia kipindi cha pili wanaume hao waliingia kwa kasi kubwa,kila kocha akifanya mabadiliko kwa mujibu ya makosa ya timu yake.

Ruvu walipata bao la pili  dakika ya 51  lililofungwa tena David Richard  na bao la tatu lilifungwa na Emanuel Matin dakika ya 62.

Kabla ya kuchezwa kwa mechi hiyo uongozi wa timu ya Jang’ombe boys ulishirikiana na wachezaji,mashabiki,wadau wao  pamoja na  timu ya Ruvu Shooting kufanya usafi kwenye nyumba za wazee Selbeni ambazo zoezi hilo lilianza saa 1:00 asubuhi.

Baada ya kumalizika kwa zoezi hilo mashabiki,wadau pamoja na viongozi wa timu ya Jang’ombe walishiriki kwenye zoezi la upimaji damu ambao ulifanyika Sebleni.