KIGALI, RWANDA

WANANCHI wa Rwanda wamepokea kwa hisia tofauti kuhusu mpango ulioridhiwa hivi karibuni na serikali ya nchi hiyo kuruhusu kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi ya kimatibabu na kiuchumi.

Kwa mujibu wa sheria za Rwanda, matumizi ya bangi nchini humo ni kinyume cha sheria, kiasi ambacho wananchi hao wamepatwa na mkanganyiko mkubwa.

Serikali imeshikilia kwamba kilimo cha bangi kitaendeshwa kwa mujibu wa sheria na lengo lake linahusu maslahi ya kiuchumi na afya hasa kuviwezesha viwanda kutengeneza dawa na kemikali za huduma ya mwanadamu kupata malighafi ili kutoa matibabu hasa watu wenye magonjwa sugu.

Waziri wa afya wa Rwanda, Dk. Daniel Ngamije aliesema kilimo cha bangi kitakuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa Rwanda, lakini kubwa zaidi kuhusu huduma bora katika sekta ya afya.

“Ukianzia na kilimo cha chai na kahawa kilimo hiki tunachokizungumzia kitatupatia nafasi ya kutuma bidhaa nje ya nchi kama zilivyo bidhaa nyingine za mazao mbalimbali na haya yataleta faida hasa kwenye sekta ya afya”, alisema waziri huyo.

Mkakati wa serikali ni kuhakikisha pato litokanalo na bidhaa zinazouzwa nchi za nje linapanda kutoka dola 465 kwa sasa hadi dola za Marekani bilioni moja za Marekani ifikapo mwaka 2024.

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya taifa ya maendeleo RDB ambayo kazi yake ni kuratibu na kuhamasisha uwekezaji wa kigeni, Clare Akamanzi alisema kuanzisha kwa kilimo cha bangi ni fursa ya maendeleo ya kiuchumi.

Mpaka sasa serikali haijabainisha ni eneo gani la nchi ambako kutaendeshwa kilimo hiki cha bangi wala kutangaza hasa ni wakati gani kitakapoanzishwa. Kwa mujibu wa sheria ya sasa, kulima na kutumia bangi ni kosa la jinai.