NA NASRA MANZI

HIVI karibuni Tamasha la Elimu Bila ya Malipo limefikia tamati katika viwanja vya Mao Zedong kwa mwaka huu,ambapo zilianzia na harakati mbali mbali za shamra shamra na ufunguzi huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Uzinduzi huo ulishirikisha michezo, kwa wanafunzi ikiwemo Sanaa,ngoma,utenzi,pamoja na nyimbo za kishujaa kutoka kwa wanafunzi mbalimbali.

Lakini pia uzinduzi mwengine ulifanyika katika mnara wa Kisonge katika maonesho ya ujasiramali, ambapo wanafunzi kutoka Vyuo vya Mafunzo ya Amali kazi wanazosomea katika vyuo vya Amali.

Hatimae zikamaliziwa kwa mbio za Nyika zilizofanyika katika uwanja wa Mnazi Mmoja,ambapo wanafunzi kutoka Unguja na Pemba walionesha ushindani na vipaji vyao, jambo ambalo limeleta hamasa katika kuimarisha michezo katika skuli zao.

Haya yote yanatokana na ushirikiano wa Idara ya Michezo kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na walimu, kwa kufanya jitihada za kuendeleza na kuinua michezo na Sanaa katika skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.

Nampongeza Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kuimarisha na kukuza Sekta ya Michezo kwa kujengwa viwanja vya michezo maeneo mbali mbali kwa Unguja na Pemba, ili wananchi wa jinsia zote wavitumie kwa kuibua vipaji vyao.

Lakini pia pongezi nyingi kwa walimu kwa kufanya jitihada   za kufundisha,hivyo ni vyema tuwathamini walimu na kuweka heshima katika michezo yetu na katika masomo kwa maendeleo ya sasa na badae.