NA KHAMISUU ABDALLAH

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema CCM ndiyo chama kilicholeta uhuru, mapinduzi ya Zanzibar na muungano kupitia vyama vya Afro Shirazi na TANU.

Samia aliyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni wa kuwaombea kura wagombea wa CCM uliofanyika katika uwanja wa mpira skuli ya Paje Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema mambo hayo lazima yaendelee kudumishwa na kuimarishwa wakati wote kwani CCM ndio chama pekee kinachoweza kuyaendeleza hayo.

Alisema CCM kila siku inasimama mambo hayo ikiwemo utawala bora, utawala wa sheria na ustawi wa jamii unaohakikisha usalama amani na utulivu ndani ya nchi ili wananchi waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi kijamii na kisiasa bila ya kubughiwa.

Makamu huyo wa rais, alibainisha kwamba CCM inatekeleza ustawi wa maisha ya watanzania kupitia ilani yake ya mwaka 2020/2025 kuona wananchi wanapata maendeleo na wananufaika na nchi yao.

Aliipongeza serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza ilani kwa asilimia kubwa ilani ya CCM kupitia sekta mbalimbali kwa maslahi ya watabzabia.

Mbali na hayo, aliwaomba wananchi wasikubali wanasiasa waliofilisika kwani serikali inajenga miundombinu mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya watanzania.

Akimzungumzia mgombea urais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi alisema amekuzwa katika maadili mema hasa katika CCM na ana sifa za uongozi kwani ni kijana mtulivu hana papara na anaeheshimu kila mtu kama anavyojiheshimu mwenyewe.

Sambamba na hayo, alibainisha kwamba mgombea huyo ni kijana mdogo mwenye mawazo ambayo yanaweza kuendelea kuibadilisha Zanzibar kimaendeleo.

Hivyo aliwaomba wananchi kushikamana na kujitokeza katika kuwapigia kura viongozi wa CCM akiwemo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli, mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wabunge, Wawakilishi na madiwani ili waweze kushirikiana katika kuleta maendeleo.

Aliwasisitiza vijana kutokubali kuuza vipande vya kupigia kura kwani itakuwa wameuza haki yako na uhuru wao kikatiba wa kuchagua viongozi wanaowataka.