SMZ, SMT zasaini hoja zilizofikiwa makubaliano

NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

SERIKALI ya Jamhuri wa muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zimesaini hati za makubaliano za kuondoa hoja tano za muungano na nyengine sita zinasubiri maamuzi ya kikao cha kamati ya pamoja ili kutolewa maamuzi.

Makubaliano yaliyosainiwa ni pamoja na ushiriki wa SMZ kwenye masuala ya kimataifa na kikanda, ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, gharama za kushusha mizigo bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar.

Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na utaratibu wa vikao vya kamati ya pamoja na SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya muungano.

Waliotia saini hoja ya kwanza ya ushirishwaji wa SMZ kwenye masuala ya kimataifa na kikanda, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi, Mwaansheria Mkuu wa Serikali wa SMT, Dk. Adelardus Kilangi na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Said Said.

Hoja ya pili ya ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilisainiwa na waziri wa Mambo ya Nje na Afrika Mashariki, Prof. Kabudi, Waziri SMZ, Gavu na Mwanasheria wa SMT Kilangi na Mwanasheria wa SMZ Said Said.

Aidha hoja ya tatu gharama za kushusha mizigo bandari ya Dar es salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar ilisaini na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania Innocent Bashungwa na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali na Wanasheria wa Tanzania na Zanzibar.

Hoja ya nne utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ilisaini na waziri wa sekta ya nishati wa Tanzania Dk. Medard Kalemani na waziri wa Ardhi, Nyumba , Maji na Nishati, Salama Aboud Talib na wanasheria wote wawili walisaini.

Sambamba na hoja ya tano utaratibu wa vikao vya kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya muungano ilisaini na katibu mkuu Kiongozi SMT, Balozi John Kijazi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa SMT, Dk. Adelardus Kilangi na Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Said Said.

Sherehe za utiliaji wa saini huo umefanyika Ikulu ya Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali iddi na viongozi mbali mbali wa serikali za SMT na SMZ.

Akizungumza katika sherehe hizo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema kutiliwa saini hati ya hoja hizo ni kuongeza uimara wa muungano wa Tanzania ili kuendelea kudumu.

Alisema kutiwa saini hoja hizo haimainishi muungano una matatizo bali unaongezwa kuwa imara na kuendelea kudumishwa kwa faida za pande mbili za serikali za SMT na SMZ, ambapo Rais Magufuli na Rais Shein wanachukuwa jitihada za kuudumisha muungano huo.

Alifafanua kuwa, Muungano huo umetimia miaka 56 ambao una tija na hamasa ya kutafutiwa ufumbuzi wa kasoro zinazojitokeza na zitazojitokeza ili kuweza kuondolewa na kuimarika zaidi, ambapo alisisitiza kuendelea kuimarisha umoja, amani na mshikamano uliowepo.

Nae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kusainiwa kwa hoja hizo kutaleta faida nyingi kwao na vizazi vijavyo, ambapo hato hiyo ni kieleleza tosha ya sekretarieti ya Kamati ya pamoja ambayo inajumuisha wajumbe wa pande zote mbili za Muungano za SMT na SMZ.

Alisema serikali zinafanya kazi kwa ushirikiano kwa maslahi ya pande zote za muungano, ambapo kwa muda mrefu wananchi wamekuwa na malalamiko ya kuhusiana na maamuzi yanayofanyika katika utekelezaji wa mambo ya muungano.

Balozi Seif alisema kuanzishwa kwa vikao vya pamoja na kushughulikia masuala ya muungano hoja nyingi zimepatiwa ufumbuzi ni pamoja na mapendekezo ya Tume ya pamoja ya fedha, usajili wa vyombo vya moto na mgawanyo wa mapato.

Alisema dunia inatambua kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa na ndio maana imeweza kupanda na kufikia katika nchi za uchumi wa kati.

Awali mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Mwinyi alisema serikali zote mbili za SMT na SMZ zitaendelea kuzifanyia kazi changamoto chache zilizobakia katika muungano kwa manufaa ya watanzania.

Alisema wakati alipokuwa waziri wa muungano mwaka 2006 – 2008 alikuwemo katika kamati hiyo ambapo hoja karibu nyingi ziliondolewa na hizo tano zimefutwa na sita zinaendelea kufanyiwa kazi ili kuja kufutwa rasmi na kamati.

Alichukuwa nafasi hiyo kuiaga kamati hiyo kwa vile ameshaingia katika kinyang’anyiro kwa kugombea urais Zanzibar, ambapo aliwaahidi serikali ijayo itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazojitokeza ikiwemo hizo sita zinazosubiri baraka ya kamati.

Nae Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipongeza kamati ya SMT na SMZ kwa kuonyesha umakini mkubwa na kuwajengea imani wananchi wa serikali zote mbili katika kushughulikia kasoro hiyo pamoja na kulinda Muungano huo, ambao ni chimbuko la umoja, upendo na mshikamano wa nchi hii.

Alisema nia ya viongozi wa serikali zote mbili wanajivunia Muungano huo kutimiza miaka 56 ukiwa bado upo imara na kuzinduliwa miradi mbali mbali ikiwemo ya miundombonu.

Alisema kumeweza kuondolewa kwa changamoto ya kodi ya thamani VAT katika umeme pamoja na kusamehewa deni kwa Shirika la Umeme Zanzibar baada ya kuingia serikali ya awamu ya tano madarakani, Dk. Magufuli.

Alieleza Aprili 26 mwaka huu sherehe za Muungano hazikuweza kufanyika, ambapo fedha zilizokusanywa Dk. Magufuli alisema zipelekwe Zanzibar shilingi milioni 500 kwa ajili ya kupambana na Corona.