RIYAD,SAUDIA ARABIA

SERIKALI ya Saudi Arabia imeregeza vizuizi vyake dhidi ya virusi vya corona na kuruhusu idadi iliyowekewa ukomo ya raia na wakaazi wa nchi hiyo kuzuru eneo takatifu la Kiislamu mjini Makka.

Mahujaji waliovaa barakoa na kutokaribiana walionekana wakiomba na kuzunguka Kaaba yenye umbo la mchemraba katika Msikiti Mkuu kuanzia mapema asubuhi.

Serikali haijasema ni kipi kilisababisha kuregezwa kwa vizuizi hivyo,lakini wachambuzi wanasema huenda Serikali inajaribu kuchechemua uchumi.

Idadi ya kila siku ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Saudi Arabia imekuwa ikipungua tangu ilipofikia kilele mwezi Juni.

Lakini kiwango cha ukosefu wa ajira nchini humo kimekuwa kikiongezeka,kwa kiasi kikubwa kutokana na janga la virusi hivyo na bei za chini za mafuta ghafi ulimwenguni.

Serikali ilisitisha hija mwezi Machi ili kudhibiti ueneaji wa virusi hivyo.

Pia ilipunguza idadi ya mahujaji katika hijja ya mwaka huu, na kuruhusu wakaazi na raia wa nchi hiyo kushiriki.

Kuanzia mwezi ujao,Serikali ya nchi hiyo inapanga kuruhusu mahujaji kutoka nje ya nchi kutembelea eneo hilo takatifu.