SANAA, YEMEN

MUUNGANO wa kijeshi unaoongozwa na Saudia na waasi wa kihouthi wa Yemen, wamekubaliana kubadilishana wafungwa 1,081 na raia wa Saudia 15, katika ubadilishaji mkubwa uliotokea tangu mwanzo wa mazungumzo ya amani.

Ndege zilizobeba wafungwa waliobadilishwa na pande hasimu nchini Yemen, zilipaa kutoka viwanja vitatu tofauti, katika operesheni ya kuwarejesha nyumbani wanaume wapatao 1,000 waliotekwa katika mapigano.

Ubadilishanaji huo ni ishara ya kuoiga hatua katika mchakato wa kumaliza mzozo uliyozuka miaka sita iliyopita nchini Yemen, ambako Wahouthi wanaendelea kudhibiti sehemu kubwa ya upande wa kaskazini licha ya uingiliaji wa Saudi Arabia na washirika wake tangu mwaka 2015.

Imeelezwa kuwa, ndege mbili zilibeba wanachama wa muungano unaongozwa na Saudia walioachiliwa kutoka kizuizini, ziliondoka kutoka uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na Wahouthi.

Ndege moja iliyokuwa imebeba wafungwa wa Saudia na Sudan, ilielekea Saudi Arabia huku nyengine ikielekea katika uwanja wa ndege unaodhibitiwa na serikali wa Sayoun katika mkoa wa Hadramount.

Taarifa zinaashiria kuwa ndege iliyobeba Wahouthi waliotolewa kifungoni na muungano huo iliondoka katika uwanja wa ndege wa Sayoun na ndege ya pili iliwasili kutoka uwanja wa Abha nchini Saudi Arabia.

Kupitia ukurasa wa twitter kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu ICRC imesema jumla ya ndege tano zimepaa kutoka viwanja vya ndege vya Sayoun, Sanaa na Abha.