NA MWAJUMA JUMA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya watoto, inaendelea na mkakati wa kuimarisha sauti za watoto kupitia njia mbali mbali ikiwemo mabaraza katika ngazi za shehia, wilaya na taifa.

Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Moudline Castico, alieleza hayo huko ofisini kwake Mwanakwerekwe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku ya mtoto wa kike inayoadhimishwa kila ifikapo Oktoba 11 ya kila mwaka.

Alisema pamoja na mikakati hiyo bado sauti za watoto zimezimwa maskulini na hata katika majukwaa ya umma, inayotokana na majukumu ya kijinsia yanayobeza umuhimu wa msichana na mizizi ya mila na desturi zinazochangia wasichana na wanawake kutothaminiwa.

Waziri huyo alisema wizara kwa kushirikiana na mashirika ya C-Sema na UNFPA yameandaa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani wakiwa wanaungana na mataifa mengine duniani ambayo ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa watoto wa kike.

Alifahamisha kwamba katika siku hiyo ujumbe wa mwaka huu ni “Sauti Yangu, ni Usawa wa Baadae”, ujumbe ambao unatoa fursa kwa jamii na taasisi zinazoshughulikia masuala ya watoto kuzingatia sauti za watoto wa kike kwa kuwasikiliza.

Kwa upande wake meneja wa huduma ya simu kwa mtoto Fatma Ahmad C-Sema alisema kuwa wana miradi wanayoitekeleza ili kuwalinda watoto wote ikiwemo huduma ya simu kwa mtoto ambayo katika uwepo wake wamegundua kwamba watoto wa kike ni waathirika zaidi katika masuala ya udhalilishaji wa kijinsia.

Hivyo alisema wameweka huduma hiyo ili kuwa rahisi kwa mtoto wa kike kutoa taarifa zao bila woga na kuunganisha na ile mifumo ya ulinzi na usalama wa mtoto ambayo imewekwa na Serikali na wadau mbali mbali.

Sambamba na hilo pia wana mradi maalumu wa kuzuia udhalilishaji wa watoto Zanzibar (KUWAZA), ambao unaendeshwa kwa ushirikiano wa pamoja na Action Aid Tanzania na Pathfinder International ambapo miradi yote hiyo inalenga usalama wa mtoto.