NA MWANAJUMA MMANGA

WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Maudline Castico, amesema serikali itaendelea kuwaunga mkono wazee kwa kuwapatia huduma ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Aliyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani ambapo hufanyika kila ifikapo Oktoba mosi ya kila mwaka hafla hiyo iliyofanyika huko ukumbi wa ofisi ya Jumuiya ya wazee Zanzibar (Juwaza 11) Mikunguni.

Alisema miongoni mwa huduma hiyo ni pamoja na kuwawekea dirisha lao la afya kwa wazee, vitambulisho vya kupandia gari, bima ya afya na matibabu bure.

Aidha alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesharuhusu matibabu bure ndani na nje ya nchi na kwamba wazee hawapaswi kubughudhiwa.

Aliongeza kusema kuwa pamoja na kuendelea kutoa fedha za pencheni kwa wazee na muda utakaporuhusu kima kitaongezeka zaidi kuwapatia wazee.

“Bila ya wazee hakutakuwa na taifa zima kwani wazee wana mchango mkubwa katika jamii, familia na taifa kwa ujumla hivyo ni wajibu wetu wazee kuwalinda”, alisema waziri huyo.

Akizungumzia suala la udhalilishaji waziri huyo alisema kumekuwa na tabia ya udhalilishaji kwa wazee hivyo amekemea tabia hiyo na kuwataka wale wote wanaofanya vitendo, hivyo kuacha mara moja na endapo watabainika hatua kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.

Akizungumzia suala la uchaguzi aliwataka wazee hao kupiga kura na kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar, Dk. Magufuli, Dk. Hussein Mwinyi na viongozi wote wa chama tawala ili kupata viongozi wanaofaa, wanaopenda nchi yao.

Naye Meneja wa Miradi ya Kinga na Kijamii ‘Help Age International’, Jecome Mwaya alisema kuwa idadi ya wazee inaongezeka kama inavyoelezwa na umoja wa Mataifa, kadiri idadi ya watu inavyozidi kuongezeka.

Hivyo serikali kuwa na ubunifu wa hali ya juu kuweka sera na huduma za umma zinazolenga watu wazee kushughulikia makaazi, ajira, huduma ya afya, miundombinu na kinga ya jamii kati ya zingine.