BAMAKO,MALI

SERIKALI ya mpito iliyopewa jukumu la kuirejesha Mali katika utawala wa kiraia imetangazwa, huku baadhi ya wanajeshi walioshiriki mapinduzi ya mwezi Agosti wakiteuliwa kushika wizara nyeti.

Kanali Sadio Camara aliteuliwa kuwa waziri wa ulinzi, Kanali Modibo Kone aliteuliwa kuwa waziri wa usalama na Kanali Ismael Wague kapewa wizara ya maridhiano ya kitaifa.

Bah N’Daw, aliyewahi kuwa waziri wa ulinzi kuanzia mwaka 2014 hadi 2015 na kushikilia nyadhifa nyengine kadhaa za jeshi, aliapishwa kuwa rais wa mpito mwezi uliopita, huku kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi, Assimi Goita akiteuliwa kuwa makamu wa rais.

Katika kutimiza ahadi yake kwa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS ambayo iliiwekea Mali vikwazo baada ya mapinduzi, Moctar Ouane ambaye ni raia aliteuliwa kuwa waziri mkuu.

Serikali ya mpito inatarajiwa kufanya uchaguzi wa kidemokrasia ndani ya miezi 18.