WASHINGTON,MAREKANI

WIZARA  ya Sheria ya Marekani imewasilisha kesi Mahakamani ya kuvunja sheria ya uaminifu dhidi ya kampuni ya Google, ikisema kwamba inahodhi soko ili kuvuruga ushindani katika masoko ya utafutaji taarifa mtandaoni na kuonyesha matangazo.

Wizara hiyo iliwasilisha kesi hiyo kwenye mahakama ya eneo la Washington DC pamoja na majimbo 11.

Maofisa wa Wizara hiyo wanaishutumu kampuni hiyo kubwa ya utafutaji taarifa mtandaoni kwa kuingia katika makubaliano na kampuni za kutengeneza vifaa zikiwemo Apple na Samsung ili kuhakikisha kwamba Google ni chaguo la kwanza kwenye vifaa vya kampuni hizo.

Google pia inashutumiwa kwa kutumia data zinazopatikana kwenye huduma yake ya utafutaji taarifa kwa ajili ya biashara yake ya matangazo.

Wizara hiyo inasema haya na mienendo mengine inaharibu ushindani na kuwadhuru walaji.

Google inakanusha madai hayo Ofisa mwandamizi wa kampuni hiyo alisema kwamba kesi hiyo ina dosari kubwa.

Alisema watu wanatumia Google kwa sababu wanaichagua, si kwa sababu walilazimishwa, ama kwa sababu hawawezi kupata mbadala.