NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Fedha na Mipango Zanzibar, Balozi Ramia Mohammed Abdiwawa amewataka watendaji wa Manispaa kushirikiana na wananchi katika kulinda na kuitunza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo misingi ya kupitishia maji ya mvua, taa za barabarani na miradi mengine muhimu ili kuepusha kufanyiwa uharibifu ndani ya maeneo yao.

Kauli hiyo aliitoa katika hafla ya kukabidhi mradi ya Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) iliyokamilika kwa tawala za mikoa hafla ambayo ilifanyika katika ofisi za Wizara Vuga.

Alisema wapo baadhi ya wananchi hufanya uharibifu wa makusudi wa miradi hiyo kwa kutupa taka ngumu katika misingi inayopitisha maji ya mvua hali ambayo inarejesha nyuma maendeleo nchini.

Aidha, alisema dhamira ya serikali ni kuona wananchi wake wananufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo ipo haja ya kuthamini jitihada hizo kwani serikali hutumia fedha.

“Shirikianeni na wananchi katika kuilinda miradi hii na waone hii miradi ni yao, kwani serikali imekopa pesa hizi kupitia benki ya dunia na zinatakiwa kulipwa,” alisisitiza.

Hata hivyo, alisema bado miradi mengine haijamalizika mtaro wa Kwabitihamran, bwawa la Mwanakwerekwe na kuona wanaelendelea kuifanyia kazi ili kukamilisha kikamilifu.

Kwa upande wa jaa la kibele alisema bado halijakamilika na kuamini kwamba serikali itakayokuja wataliendeleza na kukamilisha.

Nae, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheir, alipongeza wizara ya fedha kwa kuamua kuisimamia miradi hiyo kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.

Hata hivyo alisema miradi hiyo imesaidia sana kwa maeneo ya Unguja na Pemba, ikiwemo wananchi kupata urahisi wa kufanya shughuli zao kwa urahisi hasa katika kipindi cha mvua.

Aidha alisema wataendelea kuitunza miradi hiyo ili lengo la serikali la kuanzisha jiji na kuweka miundombinu hiyo kwa lengo la kuleta mafanikio kwa wananchi liweze kufikiwa.

“Ni imani yangu kwamba miradi mengine itakapokamilika watatukabidhi ikiwemo jaa la kibele, bwawa la Mwanakwerekwe ili kufikia lengo walilokusudia,” alisema.