NA MARYAM HASSAN
KESI iliyokuwa inamkabili mshitakiwa Robison Ismail Sambo (35) mkaazi wa Kizimkazi imeshindwa kusikilizwa kwa sababu Hakimu husika amezarulika.
Kesi hiyo imeahirishwa katika mahakama ya wilaya Mwera chini ya Hakimu Taki Abdalla Habu.
Ombi la kuahirishwa kwa shauri hilo limetolewa na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Shumbana Mbwana.
Alisema katika kikao hicho wamewasilisha shahidi mmoja lakini wameshindwa kumsikiliza kwa sababu Hakimu husika hayupo, hivyo aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikiliza ushahidi.
Robison alifikishwa mahakamani kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya ni kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria nambari 9 ya mwaka 2009, kama ilivyorekebiswa na kifungu cha 11 cha sheria nambari 12 ya mwaka 2011 sheria ya Zanzibar.
Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba tukio hilo amepatikana nalo Oktoba 23, mwaka jana majira ya saa 12:00 za jioni huko Kizimkazi Dimbani wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.
Mshitakiwa alipatikana na mkoba wa raskte rangi ya bluu kwa nyeusi ndani yake mkiwa na mifuko miwili ya plastik, pamoja na mafurushi mawili yaliyozongwa kwenye gazeti.
Alisema kati ya mfuko huo mmoja ukiwa na nyongo 41 za majani makavu na mafurushi mawili yamezongwa kwenye gazeti ambayo ni majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi yenye uzito wa gramu 252.784.
Alifafanua kuwa mfuko wa pili wa plastiki ndani yake mkiwa na kashata 17 ambazo zinasadikiwa kuwa ni bangi zenye uzito wa gramu 485.2869 jambo ambalo ni kosa kisheria.