NA HAJI NASSOR

MUFTI Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, amewataka makhatibu wa miskiti ya Ijumaa ya mkoa wa kaskazini Pemba, kuandaa hutuba ambazo zinalenga kuitunza na kuiendeleza amani iliyopo.

Akizungumza na makhatibu hao ukumbi wa mikutano Jamhuri Wete, alisema miongoni mwa majukumu yao ni pamoja na kuwaelimisha wafuasi wao dini yao juu ya umuhimu wa kuishi katika misingi ya amani.

Alisema uislamu kila siku umekua ukihimiza kuishi kwa kupendana, kusaidiana na kuoneana huruma.

Alisema kila kitu ili kifanyike kwa utulivu iwe ni ibada, kazi za amani au mikutano amani ndio msingi wa kufanikisha jambo hilo.

“Lazima sisi masheikh ambao ndio wenye wajibu ndani ya misikiti yetu kwa kutengeza na kuandaa hutuba, ni vyema hasa kwa kipindi hiki, tukaangalia suala la kuhubiri amani,”alisema.

Katika hatua nyingine, alisema lazima viongozi wa dini wawe makini na kauli zao, kwani zinaweza kusababisha athari.

Mapema Katibu wa Mufti, Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema uislamu hauna sehemu ulioamrisha kutenda maovu, hivyo ipo haja kuendeleza mema.

Khatibu wa mskiti wa Junguni Gando, Sheikh Hassan Kombo Khamis, alisema wanajitahidi kuwaelimisha wafuasi wao juu ya umuhimu wa amani lakini wanasiasa wamekuwa wakiwachanganya kutokana na nguvu walizonazo.

“Wanasiasa wanawahubiria vyengine na sisi tunawahubiria vyengine, sasa inakua tunavutiana,” alisema.

Sheikh Ahmada Ali Makame kutoka Micheweni alisema, lazima ofisi ya Mufti, ikutane na wakuu wa vyama vya siasa na kuwaeleza umuhimu wa amani.

Mkutano huo wa siku moja, ni muendelezo wa ofisi ya mufti katika kuwaelimisha viongozi wa dini juu ya kuendelea kuitunza amani.