ADDIS ABABA,ETHIOPIA

SERIKALI ya Ethiopia imepiga marufuku kuruka ndege katika anga ya Bwawa la al Nahdha lililozusha mzozo mkubwa kati yake na Misri na Sudan.

Kwa mujibu wa televisheni ya al Jazeera ya Qatar, serikali ya Ethiopia ilitangaza kuwa anga ya mkoa wa Benishangul ambako ndiko lilikojengwa Bwawa la al Nahdha, ni marufuku kuruka ndege.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Ethiopia alisisitiza kuwa, kurusha ndege katika anga ya mkoa huo kumepigwa marufuku kwa mashirika yote hata la Ethiopian Airlines.

Shirika hilo limesema,sababu iliyopelekea kuchukuliwa hatua hiyo ni kulinda usalama wa Bwawa la al Nahdha.

Limeongeza kuwa, ndege pekee zitakazoruhusiwa kupaa juu ya anga ya mkoa wa Benishangul ni zile zenye vibali maalumu vya jeshi la anga la Ethiopia.

Nchi tatu za  Misri, Ethiopia na Sudan ziliingia kwenye mzozo mkubwa kuhusu ujenzi wa bwawa hilo.

Misri inapinga vikali ikidai bwawa hilo litapunguza kiwango cha maji ya Mto Nile yanayoelekea Misri, wakati Ethiopia ikisema ni haki ya kila taifa kutumia inavyotaka maliasili za nchi yake.

Juhudi za kutatua mzozo huo zilishindikana hadi hivi sasa. Mzozo huo umepelekea hata Misri kutishia kutumia nguvu za kijeshi kusimamisha mradi huo mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme barani Afrika.

Mwaka 2011 Ethiopia ilianza rasmi kujenga Bwawa la al Nahdha. Katika hatua ya awali ilipangwa bwawa hilo lianze kufanya kazi mwaka 2017 lakini mzozo mkubwa baina ya nchi hizo tatu ulipelekea kuakhirishwa uzinduzi wake hadi sasa.